Haiwi mbingu kijani,launiye samawati
Haitawa abadani,haiwi hata katiti
Ikiwa Bin Mwaguni,labuda niwe hayati
Utakalo silifati,abadani katwaani.
Mie mja wa imani,nilofunzwa hasanati
Na kila chuo cha dini,nimesoma kila hati
Nafuata la Dayani,nilitendeto kwa dhati
Utakalo silifati,hata unganipa nini
Riyali za ki Omani,au unipe manoti
Unituze na madini,almasi kwa yakuti
Heri nitupe jaani,kuliko zako sharuti
Utakalo silifati,ahera na duniani
Unitwae ziarani,tupae na maroketi
Tutue hata mwezini,tufike huko tuketi
Sitalifuata sini,lisilo la Jabaruti
Utakalo silifati,bora kuenda mavani.
Uwaite kikaoni,adinasi na wanati
Uneke kikaangoni,na futa la alizeti
Ni budi nife motoni,kulikoni dhulumati
Utakalo silifati,na siombi samahani
Uniteke safarini,pamoja na zaujati
Unifunge mgongoni,mabomu maguruneti
Sifuati asilani,utakalo Mwanasiti
Utakalo silifati,ardhini na angani
Unijie baitini,upike maanjumati
Makuku kwa biriani,tushushe na sharubati
Nitakula yangu tani,kisha nikonyeshe geti
Utakalo silifati,nti kavu na maini
Buriani buriani,katangaze magazeti
Useme hata kwa nani,nahari wa lailati
Sishtuki mtimani,nije kupigia goti
Utakalo silifati,dhahiri na faraghani.
Rashid Mwaguni.
WRITER – RASHID
