Kuna banati mzuri, aloumbwa kuumbika

Ulimwengu mashuhuri, kila kona atajika

Urembo na utajiri, kila Mtu amtaka

Alonacho kumpoka

 

Ana milima kidari, yabusu mbingu kufika

Madini lulu ambari, pengine yasopatika

Apendeza mandhari, kila mtu amtaka

Alonacho kumpoka

 

Tabia nchiye shwari, hupendeza wote mwaka

Kwa jua la anga zuri, ling’aalo likimweka

Misimuye kuna hari, vuli kipupwe  masika

Na mitoye na Machaka

 

Manukiziye uturi, rihi ya kufurahika

Na mila na desturi, zilizodumu mikaka

Wanamuita fakiri, na mali meyalundika

Alonacho kumpoka

 

Umbo lake huyu mwari, heba ya kutamanika

Hawataki kughairi, wana kani wameshika

Wataka kumhasiri, mulukiye kumpoka

Alonacho kumpoka 

 

Kuna wengi wenye shari, wamwambao ‘badilika!’

Aache chake kizuri, afate kukengeuka

Ila naye hafikiri, bakunja wanamteka

Alonacho kumpoka

 

Mrembo nakushauri, mwenye heba Afrika

Usikengeke fikiri, sikubali kukengeka

Wakwandamao si siri, kuna jambo wanataka 

Ulonacho kukupoka

 

Nakwambia tahadhari, yao yatilie shaka

Bora wakwite jeuri, kuliko yatokufika

Waepuke mabepari, wachina na Amerika

Na wote wanokutaka, Mamaangu Afrika.

 

Copy right:Rashid Mwaguni

Categorized in: