Nilipokuwa mdogo waliniambia kua. Kua uone… Kwa hakika kipindi hicho sikuweza kuipambanua vyema kauli hii. Nami nilidhani nikue niyaone – niyaone majumba marefu niliyokuwa nikiyaangalia kwenye picha. Niyaone yale niliyokuwa nayaona kwenye kitabu cha ramani kilichokuwepo nyumbani. Wakati huo nilikuwa na akili za kitoto haswa! Kikubwa nilichojua ni kuhesabu na kuandika tu angalau imla tulizotajiwa na mwalimu Hanuni darasani kwa lugha ya Kiswahili. Naam! Hivi sasa nimekua, na nimeyaona mengi mno na naendelelea kuyaona. Lakini jambo hili limenikaa sana rohoni. Limeniganda haswa! Mithili ya mtu na kivuli chake pale mwanga unapomuakisi. Hivi ni kweli hili lilikuwemo katika yale niliyoambiwa kua uyaone au lilikuja tu kujipendekeza ili kuyachelewesha haya yaliyokusudiwa!?
Nilikuwa katika msongo wa mawazo. Ilikuwa maeneo ya Forodhani. Haikuwa kawaida yangu kwenda hapo. Lakini nilienda kupata utulivu. Majira ya saa 11 ya jioni. Nilijipumzisha katika kibaraza kimoja kilichopo karibu na ufukwe wa bahari. Binti mrembo alitokea kwa nyuma yangu na kunifumba macho. Baada ya kunifumba tu nilistuka na kuruka juu kwa hasira.
“Mpuuzi we! Watu wana stress zao unakuja kuzizidisha” nilisema kabla ya kugeuka nyumba kumwona mrembo huyo.
“Samahani” aliomba radhi kisha akaendelea “Nilikufananisha na… na… samahani sana, tena naomba unisamehe” aliomba radhi kwa unyenyekevu huku macho yake yakilengalenga machozi.
Nilipogeuka na kumwona moyo wangu uliripuka riip! na kupiga pa! nikajihisi mimi ndo mkosa kwa binti huyo mrembo mwenye unyenyekevu. Nilipogunduwa kuwa hakudhamiria ubaya kwangu, nami niliamuwa kumsamehe. Na sote tulisameheana. Mazungumzo yakaanza baina yetu. Lakini kipindi cha sekunde 30 hivi nilijiuliza… “Kwa nini rafiki zangu wengi huanza huamiliana nao kwa njia ya ugomvi?”
“Naitwa Shadida” alianza kujitambulisha huku tabasamu mwanana akiliachia. Na zaidi nilichokishufu ni vile vishimo vya mashavuni mwake alipokuwa akitabasamu.
“Wow! una jina zuri, Maa Shaa Allah” nilijibu kwa ghushui.
“Mwenzangu je?” aliniuliza.
“Majanga” nilijibu kwa unyonge.
“Haha hahaaa….. Majanga?” alicheka kwa tashtiti.
Siyo kwamba hakusikia nilichokisema nahisi alilishaangaa jina langu. Siyo yeye tu na wengine wengi hulishangaa jina langu. Hata mimi nalishangaa pia. Wazazi wangu walikosea mno kuniita jina hili, lakini…
“Naomba soda 2” Shadida alimuagiza muhudumu aliyepita mbele yetu.
“Kwa nini unacheka?” nilidadisi.
“Jina tu limenifurahisha”
“Zuri!?”
“Sana, zuri kama mwenye jina”
Nilizidi kubaini kuwa Shadida hakuwa na nia mbaya kwangu. Hakunivunja moyo. Ni mtu wa kwanza kunitamkia kwa lisani yake kuwa jina langu ni zuri.
“Karibu soda” alinikaribisha.
“Ahsante” nilijibu na sikuinywa kwa muda hivi.
“Unaiogopa au hutumii!?” alidadisi.
“Sijuwi”
“Kwa nini hujui”
“Sijawahi kunywa hata siku moja tangu nizaliwe” nilijibu.
Majibu yangu yalikuwa yanamfurahisha na kumpa faraja. Alijuwa namfanyia mzaha na futuhi. Lakini ulikuwa ni uhalisia na ukweli mtupu.
“Basi jaribu naamini utaifurahia, au nikinywishe?”
“Hapana, bado sijawa kilema na utamu wa jambo ufanye mwenyewe”
Aliniangalia sana, huku tabasamu halikumkauka usoni mwake.
“Naishi mtaa wa Malindi, mwenzangu?” alizidi kunidadisi kwa maswali huku tukiyalainisha kwa soda baridi aina ya Fanta.
Swali lake lilinitia kigugunizi cha ghafla. Lakini maneno yake hayakunitia shaka hata kidogo. Muonekano wake unadhihirisha wazi kuwa anaishi maeneo ya Malindi. Yanayosemwa kuwa yana watoto wastaarabu.
“Mwembe Makumbi” nilimjibu kwa kuona aibu huku nimeinamisha kichwa chini.
“Hivi Mwembe Makumbi ndiyo Chumbuni?”
“Kwa nini?” nilimbandika swali kabla ya kujibu la kwake.
“Ah! Kuna shoga yangu anaishi Chumbuni ila sijawahi kufika huko, anaitwa Raya bint Swaleh, nilisoma naye skuli ya Forodhani”.
Moyo uliniripuka mripuko wa ndani kwa ndani baada ya kulisikia jina la Raya likitajwa na Shadida. Nilijikaza. Nikayakomesha macho yasitoe machozi. Na mwili nikauambia jikaze. Kiukweli ilinichoma mno ila sikutaka kuonesha hisia hasi mbele ya mrembo Shadida.
“Ah! Ni mtaa wa karibu tu kama Malindi na Darajani”
“Raya unamjua?”
“Simjui” nilijibu kinafiki.
Kwa hakika Raya namjua. Yeye ndiye sababu namba moja iliyonifanya kuja Foro ili niweze kupunguza msongo wa mawazo. Raya alikuwa mchumba wangu, ila kwa sasa tumeachana. Ameniacha eti kwa sababu amepata bwana mwengine. Basi nilijifanya simjui kwa wakati huo. Shadida alinipatia business kadi nami nilimtilia namba zangu kwenye simu yake. Alinihadithia mambo yote aliyofanyiwa na Raya. Ingawa walikuwa ni marafiki lakini walifarikiana. Na kilichowafarakanisha ni mapenzi tu. Ndiyo mapenzi. Yanauma, yanakera, yanasumbuwa kwa upande hasi, na kwa upande chanya hakuna asiyeyajua.
“Raya alithubutu kunichukulia mchumba wangu hivihivi”. Aliniahadithia.
Shadida hakuonekana mwenye mawazo sana kama mimi. Sijui kwa nini. Labda kwa uzuri wake. Kwani muda wowote anaweza kutokea mtu na kupendana nae.
“Nakupenda Majanga” alitamka. Kaulu yake hii ilinifanya niishiwe nguvu na kile kigugumizi kilichokuwa kikinijia hakikuwa kigugumizi tena, kiligeuka na kuwa kitata. Sikuweza kujibu chochote. Siyo kama sina shauku ya kuwa na mpenzi. Lakini nilimkumbuka salata wangu Raya. Usaliti uliyoniumiza na nikahofia kujirejea hayo kwa Shadida. Chambilecho Rakhyl alipoimba “YAMENIREJEA MAUMIVU”. Lakini pia hadhi yangu na Shadida hazilingani kabisa- hata kidogo.
“Mbona hunijibu au nimekukwaza”
“Hapana, ahsante nami nakupenda pia” nilijikaza kisabuni ili asigunduwe yale niliyonayo moyoni mwangu.
Basi hadithi ziliendelea kati yetu. Kutahamaki saa 1 ya usiku. Lakini hakuna aliyehisi kabla, kuwa sasa usiku unaaza kupiga hodi kwa jinsi mazungumzo yetu yalivyokuwa matamu na ya ucheshi. Shadida alishikwa na choo kidogo. Aliniaga kwenda msalani. Baada Shadida kuondoka mara nilivamiwa na watu watatu nisiowajua. Walinivuta na kunikokota kwa nguvu mpaka kwenye kichochoro kimoja hivi nyuma ya jengo la Ngome Kongwe. Walinipiga kisawasawa. Walinichambuwa kama karanga. Mwili wote ulinyong’onyea.
“Nimefanya nini?” niliuza.
“Hukijui?” walirudisha swali huku wakinipiga mno.
“Tulikuwa tunakuangalia tu, unamjua yule uliyekuwa umekaa naye pale, yule ni mchumba wangu… Shadida… Shadida”.
“Mchumba wako!?”
“Ndiyo, na tena iwe mwanzo na mwisho leo kukuta ukiwa naye pamoja”
Waliendelea kunipiga mpaka nikapoteza fahamu. Sikujuwa chochote kilichoendelea.
Kwa kuwa Wazanzibari wamejengwa na tabia ya ukarimu na huruma. Bwana mmoja aitwae Abdul-hamid alinichukuwa na kuniwahisha hospitali ya Mnazi Mmoja. Baada ya saa kadhaa fahamu zilirejea. Fahamu ziliporejea nilimwona mama yangu kuliani kwangu. Na nilipogeuka kushoto nilimwona Shadida. Ulikuwa ni usiku wa saa 3:30. Masikini Majanga miye! Nililazwa kwa muda wa wiki mbili bila ya kusema chochote. Baada ya hapo nilipewa ruhusa ya kurudi nyumbani. Mambo yote yalienda kwa ishara au kuandika kwenye karatasi. Shadida alinipenda sana. Nami nililijuwa hilo. Maana alikuja nyumbani Mwembe Makumbi kuniangalia kila baada ya siku mbili. Lakini mazungumzo yalifanyika kwa ishara tu. Aliniandikia maneno matamu kwenye karatasi. Mara alinichorea makopa na maua kuonesha ishara ya upendo wake kwangu.
Moyo wangu ulikuwa una hofu juu ya mambo matatu. Kwanza nilikuwa bado nampenda Raya, pili hadhi yangu na Shadida hazifanani na tatu kuhusu vitisho vya mchumba wa zamani wa Shadida.
Ama kweli mapenzi ni upofu. Baada ya siku chache niliyasahau yote hayo. Shadida hakujali hali niliyonayo. Aliridhika si haba. Alichokihitaji kwangu ni furaha, faraja na mapenzi ya dhati. Vyote hivi alivipata. Ndiyo! tena bwerere.
Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Pesa na cheo ghafla vilizima upatikanaji wa mambo hayo baina yangu na Shadida. Ahmed anayeishi mtaa wa Vuga alikuwa na cheo kikubwa serikalini. Pia alikuwa na uwezo mkubwa wa fedha. Ahmed ndiye aliyekuwa mchumba wa Shadida hapo awali. Kutoka na uwezo wake aliweza kuwarubuni mpaka wanawake wa ng’ambu akiwemo Raya. Fedha zake aliziwekeza kwenye anasa za kidunia badala ya miradi ya kimaendeleo. Na alifanya hivyo makusudi.
Ilikuwa saa 11:30 alfajiri. Siku hiyo nilijiandaa kwenda Maruhubi kufanya kazi ya kubeba dagaa. Raya alikuja nyumbani kuniomba msamaha. Nami nilimpuuza na kuondoka. Nilipofika kibaruani, simu yangu iliingia arafa. Arafa ilitoka kwa Shadida.
“Baada ya salamu, naomba leo tuonane saa 10 jioni, nina shida na wewe”
“Wapi?”
“Garden”
“Sawa”.
Muda ulipofika tulionana kama tulivyokubaliana.
“Samahani sana” Shadida aliazisha mazungumzo kwa kuniandikia kwenye karatasi maana sikuweza kuzungumza tena tangu nilipopigwa.
“Samahani ya nini tena mrembo” nilirejesha jibu kwa mwandiko.
“Ahmed kanitishia niachane nawe, bado ananipenda, na ameshakwenda nyumbani kuniwekesha- na posa ipo karibu”.
“Sasa mimi nifanyeje” nilirejesha mwandiko.
“Tutoroke”
“Twende wapi?”
“Popote”
“Popote ndo wapi? Mimi siwezi, hiyo ni hatari”
“Nakupenda Majanga, siwezi kuolewa na mtu katili kama Ahmed”.
“Usiseme hivyo, huwenda amebadilika sasa, amemaliza ujana wake” nilirejesha mwandiko kwa uchungu mno.
“Kama na wewe hunitaki sawa, lakini pia siwezi kuolewa na Ahmed”
“Bahati hiyo wenzako wanaililia, ndoa kwa mtoto wa kike hivi sasa ni bahati, nenda kaolewe…nimekuruhusu….Mungu akubariki”
Sikutaka kupoteza muda sana. Mazungumzo yenyewe yalikuwa kwa shida maana mpaka niandike. Basi yalinizidishia maumivu. Maumivu mara mbili.
Niliondoka kwa hasira. Sema tu niliweza kudhibiti hasira zangu. Nilipofika nyumbani niliigiza kuwa nipo sawa tu. Lakini maumivu niliyonayo ni mara mbili zaidi. Basi ule msemo kua uyaone ukawa unaendelea tu kujidhihirisha katika kila hatua yangu ya maisha. Nilijipa matumaini kuwa- wakati sijafa riziki zangu zipo tu. Raya na Shadida hawakuwa riziki yangu.
Sekunde hazikusimama. Kila zilipotimiza ule mzunguko wake ziligeuka na kuwa dakika, dakika zikatengeneza saa, saa ukatengeneza usiku na mchana. Usiku na mchana ukaunda siku. Baada ya siku chache harusi ya Shadida na Ahmed ilifungwa. Harusi yao ilikuwa bambam. Haikuwa ya kitoto. Sherehe ya harusi yao ilifanyika katika hoteli takatifu hapa Unguja. Hoteli VERDE. Naam! Verde iliyopo Maruhubi. Na fungate waliimalizia kwenye ABLA BEACH APARTMENTS iliyopo Beit el Ras. Siyo kwamba Ahmed hakuwa na nyumba ya kukaa. Anazo sita. Nne amezikodisha. Moja wanakaa wazazi wake na ndugu zake. Na moja anakaa yeye. Na nyumba zote hizo zilikuwa nyumba kwelikweli, siyo kama kibanda chetu kilichopo Mwembe Makumbi. Ng’ombe wawili walichinjwa kwa ajili ya karamu ya harusi yake. Mchele haukuwa mapembe bali ulikuwa ule ulionyooka kama alifu. Maneno ya vijana moja ya Kiarabu. Ahmed alijiweza na kujipata. Kufanya hivyo kwake kama kumsukuma mlevi pembeni mwa njia. Nenda urudi, zunguka kote ulimwenguni. Huwezi kukuta duka likiuza furaha na upendo. Baada ya siku saba za harusi yao. Shadida alinitumia ujumbe kwenye simu yangu. Sikumjibu. Niliupuuza na kuuwach kama ulivyo. Niliusoma juujuu tu. Ujumbe wenye kuvuta hisia kali za mapenzi.
“Ananitafutia matatizo, kwani hajui yeye ni mke wa mtu, mtu tajiri mwenye vyake na mke ndo yeye” niliwaza.
Nilichukua maamuzi magumu sana ya kuzima simu yangu walau kwa mwezi mmoja. Lakini haikuwa suluhisho. Shadida alinifuata hadi nyumbani. Sasa halikuwa tatizo ila ni majanga, mithili ya yale aliyoyaimba Snura Mushi. Nilimkataza hakunisikia. Nilitamani kuhama. Nihamie wapi? Sinapo. Hata nikihama nimkimbie mama kwa sababu ya Shadida!?. Nilijipa matumaini na kumwomba Mungu kila dakika juu ya hali iliyonikabili.
Hali ilizidi kuwa mbaya kwangu. Nilithubutu hadi kumshitaki Mungu kwanini aliniteta duniani. Nilisahau kuwa YEYE ana majaribu kwa viumbe wake. Zaidi lililonitia majonzi ni pale Raya alipokuja nyumbani kudai ana ujauzito wangu. Raya hakuwa na aibu sini. Alinibambikiza dhambi nzito isiyonihusu. Fauka ya hayo Raya alikuwa bado ni mwanafunzi wa kidato cha tano. Ikawa kesi juu ya kesi. Huku Shadida naye ananifata kila uchao. Nilihisi dunia imenielemea. Hapo nikathibitisha kuwa dunia duara na pia inazunguka. Na sasa imezunguka kwangu.
“Nifanye nini au ndo nimezaliwa Majanga?” Nilijisemea huku machozi yakifanya michirizi mithili ya mto Nile katika mashavu yangu. Msongo wa mawazo ulinikumba huku nikitembea kutoka kazini kwangu Maruhubi kubeba dagaa. Ghafla nilishtushwa na kofi zito lililoanguka nyuma ya kisogo changu. Kugeuka kumbe alikuwa Ahmed.
“Kwa nini unanichukulia mke wangu?” alifoka kwa hasira.
Sikuweza kujibu kwa kitata alichoniachia siku ile waliyonipiga Forodhani. Sikukubali. Nami nikakunja vyanda vyangu ili kutengeneza mviringo wa kiganja. Tulipigana. Nilimmudu hasa maana alikuwa peke yake tafauti na siku ile tulipokuwa Foro. Nilimdunda vizuri. Mara nilisikia “Kaa!” mfupa umekatika.
“Ananiuaaa” Ahmed alitoa usiyahi mkali.
Nilikimbia mbio kuliko za farasi. Ghafla nilikamatwa na mtu nisiyemfajamu. Ila kando kidogo na sehemu ya tukio. Bila shaka hakuja kilichotokea.
“Kulikoni, mbona mbio tena kijana, tunashtuana bure” aliniuliza. Nami sikumjibu kitu.
“Una jeuri eeee, nakuuliza hunijibu” alilalama.
“Siwezi kusema” niliandika kwa jiwe chini ya sakafu.
Baada ya hapo nilimuhadithia yote yaliyonisibu juu ya hali yangu hii. Sikuacha kitu. Mpaka hili lilonikuta hivi punde baina yangu na Ahmed. Alinitoa wasiwasi. Alinisaidia kunipeleka hospitali kwa tatizo langu la kutoweza kusema. Alinipa matumaini nitapona. Naam! Alinisaidia na tatizo likaondoka. Niliweza kusema. Tena zaidi ya mwanzo. Kila neno lilikuwa na pupa ya kuwahi kutamkwa ndani ya kinywa changu. Nashukuru nimepona. Matumaini niliyaona kwa mbali. Kumbe ni mwanasheria. Siku ya Jumatatu alikuja nyumbani kujitambulisha kiundani. Basi tulianza mazungumzo.
“Naitwa Mtatuzi, naishi Magomeni” alijitambulisha.
“Oh! Karibu sana baba” mama alimkaribisha karibu ya ndani maana Mtatuzi alikwisha ingia.
“Huyu ni mama yangu, tunaishi wawili tu hapa” nilimfahamisha.
“Anaitwa nanii?”
“Aaa… Mhhh. Amina” nilijibu.
“Na wewe Muhammad?” alinidadisi.
“Kwani umelisahau jina langu?”
“Nakutania tu maana Amina alimzaa Muhammad ambaye ni mtume wa mwisho”. Sote tulicheka kwa mzaha. Tulifahamiana tangu siku hiyo. Mtatuzi akawa kama baba yangu. Alinipenda sana. Ingawa ni siku chache tu tulizojuana lakini alifurahishwa na tabia zangu. Kwa sasa nipo katika mikono salama.
Siku ya Jumaatatu askari wawili walikuja nyumbani kunikamata.
“Nna kosa gani!?” niliuliza kwa mshangao.
“Huna kosa, sema una makosa” walishadidia.
“Mangapi?”
“Wee twende utajua kituoni”
Mama yangu alihamanika. Asijuwe la kufanya. Alituandama mwishoe alichoka na kurudi nyumbani. Si haba njiani alikutana na Mtatuzi.
“Usijali mama mambo yote nayajuwa, mwanao hana kosa hata moja”
“Mbona askari wamemkamata kama hana kosa?” huku machozi yanamchirizika.
“Wamemchukua kwa ajili ya uchunguzi tu, ila usijali yupo katika mikono salama”.
Nilikamatwa kwa sababu ya makosa matatu, mosi ni ujauzito wa Raya, pili kumchukua mke wa Ahmed na tatu ni kumpiga na kumvunja mkono Ahmed. Siku ya Jumanne nilipandishwa kizimbani. Mashtaka yangu yalisomwa. Ghafla niliinua sauti nilipopewa nafasi ya kujitetea.
“Namshukuru Mungu kuninyima mali na fedha na kunijaalia upendo na huruma”.
Baada kusema maneno haya, Raya alianguka chini. Uchungu wa mimba ulimjia. Lakini haukuwa wa kuzaa. Ujauzito wake ni wa miezi mitatu tu. Ahmed kaacha mdomo wazi. Wote walidhani siwezi kusema. Basi niliyasema yote. Kuanzia utandu hadi ukoko. Sikusaza kitu. Mtatuzi nae alikuwa wakili wangu na aliniunga mkono. Nilishinda. Jaji aliamuwa kesi kwa haki baada ya kusikiliza pande zote. Masikini Ahmed. Kumbe alikuwa na wake wawili, Raya mke wa nje ambaye ni mwanafunzi na Shadida mke wake halali wa ndoa. Loh! Dunia kizungumkuti. Usipokuwa mcharukaji utatupiwa zigo lisilokuhusu.
MWANDISHI: OTHMAN AME HAMZA
LAKABU: MFUNGWA HURU
MAHALI: CHUNBUNI – ZANZIBAR
MWAWASILIANO: 0776820608
BARUA-PEPE: othame10@gmail.com
WRITER – OTHMAN HAMZA
