Ndivyo walivyo. Na ndivyo wanavyokuwa. Wanapokuwa wadogo hutembea na kucheza pamoja. Kuchokozana, kutaniana na kupigana ndiyo michezo yao ya kila siku. Lakini ni waoga na wanyenyekevu sana kwa wakubwa zao isipokuwa wachache tu! wale wanaosemwa kuwa wameshiba maziwa ya mama zao. Samaki mkunje angali m-bichi. Methali hii husemwa sana kukumbushwa wale wanaowasimamia, kuwatunza na kuwalea. Siyo kwamba wao huwa hawaisikii methali hii, la hasha! lakini yumkini huwa hawajui kile kimaanishwacho. Wapo waliyopo mijini lakini pia wapo waliyopo vijijini. Tafauti ni mazingira tu lakini miamala ya mafunzo kwao huwa ni yayo kwa hayo. Mji hauna mwenyewe na vijiji vimejaa wahamizi walioshindwa na maisha huko mjini. Sina uhakika na kauli hii lakini kwao wao hawajui mji wala kijiji. Walipo huishi tu. Wanachohitaji ni amani, upendo, na usalama wao. Lakini tukumbuke pia huwa wana siri nyingi sana nyoyoni mwao na kukutana na mengi kama yalivyomkuta Mjaka bin Mambotele anaeishi jirani na Kijiji Cha Yaoneni.
*
Kama ilivyo kawaida ya watoto wa vijijini kutengeza manati na kwenda kuwinda ndege. Jambo hilo alilipenda sana Mjaka. Kila ifikapo siku ya Jumapili watoto hukusanyika, na kwenda kwa pamoja kutafuta ndege. Ilikuwa ni desturi yao, kushindana kuhesabu kwa kila mtu ndege wangapi aliowapata tangu walipokwenda hadi wanaporudi. Siku hiyo Mjaka alitoka peke yake kwenda mawindoni. Hakuna mtoto yoyote aliongozana nae, isipokuwa kwa mbali kaka yake alimuona akitoka na panda yake huku mifuko ya suruali lake imetuna kwa towe zilivyojazana. Alikuwa na umri wa miaka kumi lakini umbo lake halikulingana na umri wake kwani Mungu alimjaalia urefu, mwembamba na mwenye ngozi nyeusi iliyokoza tititi kama chungu kilichopikiwa kwa muda mrefu. Alikuwa sio mwoga kama watoto wengine, alijiamini kama mtu mzima. Alithubutu kuingia machaka makubwa makubwa katika uwindaji wake. Mara alikutana na chatu, mara kenge, nyoka lakini hakuwaogopa. Alikuwa akikatiza vipuu, mito maziwa yaliyotuama maji bila woga. Chambilecho Waswahili “safari hatua”. Mjaka alifika katika ziwa ambalo lipo nje kidogo na kijiji chao. Siku hiyo hali ya hewa ilikuwa shwari, maji yametulia tuli, miti inang’ara kwa mauwa, na haukuwa mng’aro tu bali ilikuwa yakiwakawaka na kumemetuka mithili taa za diskolaiti. Ndege aina kwa aina walipaa, kutua, kupita na kupituka katika ziwa hilo. Miti ya ziwa hilo ilikuwa sio mikubwa na hasa ilionekana kuota maeneo yenye tope. Alimuona ndege mzuri ambae hakuwahi kumuona katika maisha yake, alistaajabu uzuri wa yule ndege. “Mashaallah! kweli mungu ni hodari kwa kuumba, ni ndege wa aina gani huyu”.
Punde alikata shauri “siondoki mpaka nimpate ndege huyu”.
Mjaka alianza kumvizia, kumnyemelea nyelinyeli ndege huyo bila parakacha zozote.

********************************

Alijongea karibu na mziwaziwa uliopo kando kando ya ziwa hilo ambapo ndege huyo mzuri alionekana kubarizi juu ya tawi. Kila alipomsogelea tamaa ya kumpata ndege huyo ilitia fora katika moyo wake. Ziwarde aliimba kwa sauti nyororo isiomkwaruzo “swii swii swii”. Sauti iliyoongeza huba, haiba na tamaa kwa Mjaka. Alijitahidi kumsogelea pasi na kujali matope yaliofunika gubigubi ziwani hapo. Ghafla alijikuta katika ulimwengu mwengine usio wa kawaida mithili ya mtu kuzimu. Alishangaa sana… “Nipo wapi? Kwa hakika hiki ni kiini macho, wameniroga, lakini…” Mara sauti nzito ilisikika kwa nguvu za ajabu ikisema “Toka! toka! toka haraka ziwani hapa…”

Bila kutanabahi kimaanishwacho juu ya sauti hiyo, Mjaka alitetemeka huku mapigo ya moyo yakienda kwa kasi mno. “Ah! sauti ya Bibi , Bi Mwantakaje, nipo wapi jamani!”. Ilikuwa ni sauti ya Bibi yake ambaye alifariki mwaka uliopita. Sauti hiyo ilimjia katika bumbuwazi la ruya iliyochanganyika na maruweruwe ya tamaa. Aliipuza na kuhisi kuwa kuna pepo tu limempanda kichwani. Kwake alihisi kama njozi tu, tena sio njozi tu bali ni Njozi Iliyopotea ya C,G.Mung’ong’o.
Baada ya lepe la bumbuwazi, Mjaka alijizoazoa, alijikongoja na kujikokota ili kumfikia ndege huyo. Lakini loh! kudura yashinda jitihada… au tusemavyo kuwa kisu kimegonga mfupa. Hakukata tamaa , alipiga moyo konde na kujifariji kwa kusema “maisha safari ndefu ukinyimwa ya mchana utapata ya usiku…”
Alijisahau kama yupo ziwani, alizubaika na kurubunika na uzuri wa manyoya ya ndege huyo. Ama kweli ukitaka kizuri dhurika. Miguu yake ilianza kufa ganzi, mwili ukanyong’onyea, kichwani kizunguzungu, na machoni mwake aliona vimulimuli. Punde tu ndege huyo alitoweka. Mjaka hakujua afanye nini. Simanzi na majozi yalitamalaki katika nafsi yake. Aligunaguna kwa kwikwi zilizompalia “hig! hig! hig!” hatimae alidondosha chozi. Macho yalipiga wekundu kama aliyelishwa pilipili.
Mvua kubwa ilinyesha, mvua na ngurumo vilizidi kumtia hofu. Maji yaliaanza kujaa zaidi na zaidi, miguu yake ilinasa topeni. Alitumia saa tatu kupiga hatua moja mbele. Ikawa tafrani , hakuamini kilichomtokezea, aliporoja kwa uchungu “Tamaa mbele mauti nyuma…Neno ningejua huja mwisho wa safari…
Alifikiri maneno aliyokuwa akiambiwa na kake yake. Alikumbuka vyema maonyo aliyopewa. Tena alipopewa alioneka msikivu lakini utekelezaji sifuri. Angalau utasema sifuri ina thamani lakini kwake utekelezaji wa maonyo hayo hakuwa nao. Alifikiria sana hasira za kaka yake. Mara aliuhisi uso wa kaka yake upo mbele yake. Umevimba na kuvimbiana mithili andazi lililoumuka kwa hamira. Uso umebadilika kama chui. Umekunjana kama wa kizee cha miaka tisini.
“Wewe mtoto husikii kwanini? Mtazame macho yamekuparama kama mchawi muanguka na ungo. Kazi kuzurura tu huna kusoma, huna kwenda madrasa, huna kudurusu masomo yako, huna…. huna…” Alihisi kusimbuliwa na kusimangwa sana na kaka yake asiyekuwepo. Alitamani azame, azame asione kitu, kitu wala mtu yoyote, yaani awe ameihama dunia moja kwa moja. Lakini wapi hana jinsi, maji yakimwagika hayazoleki. Alipiga moyo konde. Mara aliona kivuli cha mama yake ambaye hakuwahi kumuona tangu azaliwe. Sijui alimjuwaje “Mwanangu! nani aliekukamata hapo, asiyekuachia uende, tuseme hizo tope? La sio tope, nani aliekukamata Mwanangu?” , Mjaka alishangaa sana na kuanza kuipanga familia kichwani mwake. Haidari Kheri na Mjaka bin Mambotele. Inawezekanaje tuwe ndugu au ndugu wa mama tu?. Au waliniokota baada ya mama yangu kunitupa?. Masikini Mjaka aliwaza hata visivyokuwepo, ndiyo visivyokuwepo na kuvipamba kwa utamu wa lugha kwa kuwa tayari alikuwa katika hilaki inayomkeketa maini.

********************************

Alitamani kupata msamaria mwema. Lakini muda wote hakuna mtu aliyepita Ziwani hapo. Watu wa Kijiji hicho hawakuwa wageni sana na vitisho vitokanavyo na ziwa hilo. Mjaka alikata tamaa ya kuwepo tena ulimwenguni
Ilikuwa majira ya saa tisa na nusu. Hofu na wasiwasi vilianza kumvaa kaka yake Mjaka, Haidari. Aliwaza na kuwazua. Alijiuliza maswali ambayo hakulipata jawabu lake. Mara mawazoni ikampitikia “isijekuwa amemezwa na chatu?” Mara alijiaminisha kuwa ndugu yake hawezi kupatwa na hali hiyo. Ikawa kuna msongo wa mawazo yanayomla roho na kugonga kisawasawa kichwani mwake. Haidari alikata shauri kwenda kumtafuta ndugu yake. Jambo hili lilikuwa kama ilhamu tu kwake kumpitia. Alipita na kulipituka chaka kubwa lililotenganisha Kijiji chao na Kijiji cha Yaoneni. Kusogeasogea mara alistuka kumuona mtu amezama nusu katika matope. Alikuwa ndugu yake, ndiyo ndugu yake, Mjaka bin Mambotele. Alifadhaika, mara alitaka kwenda kumuokoa, mara alirudi nyuma, kichwa kikawa kinamduru. Alipojaribu kutia mguu tu alihisi kusisimkwa mwili mzima mithili ya mtu kupigwa shoti. Alitoka mbiombio kwa usalama wake. “Masikini ndugu yangu nini kimekusibu? angalia hapo huna kauli, hafurukuti, huna mwendo, huna… huna… Masikini… Masikini” alilalama. Mara akatanabahi kupiga simu kituo cha polisi cha kati katika Kijiji chao.

“Haloo Afandi! Haidari nipo kando ya Ziwa la Mezameza katika Kijiji cha Yaoneni kuna kijana amezama kwenye tope”.
“Sawa” afande alijibu.
Mara gari la Askari waokozi liliingia kwa tifutifu la kutifua vumbi. Walishuka Askari watatu, na dereva kusalia ndani ya gari hilo. Baada ya uchunguzi na upimaji usiorasmi Askari wawili waliingia Ziwani kwa ajili ya uwokozi. Usilolijua sawa na usiku wa kiza. Kila walipomkaribia walididimia, kudidimia na kuzama kabisa. Wakawa haonekani kama barafu lililoyeyuka. Haidari, dereva na Askari aliyesalia walishangaa mno kuona tukio hilo.
“Ah! wamedidimia, wamezama na wamekwenda wapi?” dereva aliuliza. “Kusikojulikana” Haidari alijibu kwa mzaha.
Wote hawakuamini kilichotokezea. Mara Askari alipiga simu Manispaa ili kupatiwa kijiko kwa ajili ya uwokozi. Punde tu Kijiko kilifika. Kwa kuwa haikuwa mbali na alipozama Mjaka Kijiko kiliweza kuingia. Maringi ya Kijiko hicho yalikuwa na urefu wa futi kumi. Ghafla Mjaka aliweza kutoa kauli “Nakuombeni msihangaike, msipoteze nguvu zenu, roho zenu, mali zenu bure…Chunusi…Ziwani…pana Chunusi ziwani hapa, na mimi ni wa kufa tu”. “Chunusi!?” Haidari aliuliza kwa mshangao swali lisilojibu.

********************************

Haidari alianza kububujikwa na machozi, machozi khasa hatimae kilio cha kuomboleza “Kila siku tunakwambia lakini u mkaidi, husikii unaona yaliyokukuta sasa, nusu u akhera nusu u duniani”.
Dereva muongoza Kijiko alijitahidi kadiri ya awezavyo. Alijitutumua, aliamini akifanikiwa kumuokoa atapanda cheo kazini, kwani katika Kijiji chao mtu alipanda cheo na hadhi kwa kazi sio alama na mabamba ya skuli wala vyuo vikuu. Na alifanikiwa kweli, kweli na kila aliyekuwepo pale alishuhudia. Lahaula! usiombe yakufike, bora uyashuhudie tu yakitokea kwa wengine au usubiri kusimuliwa. Aliipotolewa tu Mjaka alikimbia. Sijui nguvu alizipataje na kutokomea kusikojulikana…

Jina: Othman Ame Hamza
Mwanafunzi kutoka Kampasi ya Betrasi
Hadithi hii ni kwa aijili ya shindano la CHAWAKAMA-SUZA 2019/20
Simu: 0776820608
othame10@gmail.com

WRITER – OTHMAN HAMZA

Categorized in: