Siachi na sitaacha, univae ubunifu

Nizitunge kwa papacha, kundini niweke tifu

Na mafumbo kuyaficha, ‘siwe mepesi ja difu

Najijuwa mpungufu, kuandika sitaacha

 

Siachi na sitaacha, siyo  kama najisifu

Ghassani nipa m’bacha, nifunze umakinifu

Hata moja ‘sijewacha, nipa mengi yanikifu

Najijuwa mpungufu, kuandika sitaacha

 

Siachi na sitaacha, kutunga kwa unadhifu

Tatunga kila kukicha, japo mawazo hafifu

Nimfikie Mwanacha, kwa tungo kuzisarifu

Najijuwa mpungufu, kuandika sitaacha

 

Siachi na sitaacha, kutunga bila ya rafu

Hila zenu sitazicha, maoni yenu machafu

Nikishindwa kuchekecha, Bashiru nipige tafu

Najijuwa mpungufu, kuandika sitaacha

 

Siachi na sitaacha, niwezeshe Ya Raufu

Nitumie lugha picha, kasrini waishufu

Itopekechapekecha, Mwana alicheze dufu

Najijuwa mpungufu, kuandika sitaacha

 

Siachi na sitaacha, kutunga tungo lufufu

Hata ziumie kucha, sitajali usumbufu

Niwe kama wangu pacha, Dillah kwa umaarufu

Najijuwa mpungufu, kuandika sitaacha

 

Siachi na sitaacha, labda nikiwa mfu

‘tajifikichafikicha, niingie kwenye safu

Sharifa ‘sijejificha, wewe kuti miye dafu

Najijuwa mpungufu, kuandika sitaacha

 

Othman Ame Hamza

Mfungwa huru

Donge, Zanzibar

0776820608

othame10@gmail.com

WRITER – OTHMAN HAMZA

Categorized in: