Barafu ya moyo Saumu.
Ni miaka mitatu sasa tangu uliponibwagia zani na kuniacha katika njia panda. Mbele siwezi kwenda na nyuma sitamani kurudi. Nipo tu kama mtu aliyekatwa miguu. Isitoshe, ni karibu mwongo mmoja tangu tule yamini kutunziana penzi letu lije jua ama mvua. Kumbe zilikuwa ahadi za Kiswahili tu? Ahadi zisizokwenda kwa dobi zikatakasika? Yamkini ilikuwa michezo ya utotoni tu ambayo ilikosa mashiko pindi tulipovuka daraja la utotoni na kutia maguu katika himaya ya utu uzima? Siamini. Tulijitia kuyakuza mapenzi tusiyoweza kuyamudu wakati wa mitihani. Jinsi tulivyoyaweka hadharani kama kibatari, yakaangaza kote kote. Tuliwakera waliotuonea kijicho kwa jinsi tulivodeka hadharani tukiwa sako kwa bako. Wengine walijasiria kutupagazia Uromeo na Ujulieti. Lakini tufani ya majaribu iliposibu na kutukabili, kibatari cha nyonda zetu kikazimishwa kwa mpigo mmoja.
Tazama natekwa na taathira ya kumbukizi ya kadhia iliyonifika. Naghafilika. licha ya kujishajiisha kuwa sitakubali kuongozwa na hisia zangu. Hisia zangu zishachukua hatamu za uongozi wa akili yangu tena. Mara ya mwisho kufanya hivyo, hisia zangu ziliuchubua moyo. Moyo uu huu ambao nilikuwa nimejisabilia kukupa. Tazama sijakuamkia kwenye waraka huu nilivyokuwa nimeratibu akilini. Hisia zenye hasira zilinitangulia tena! Zikavuruga mpangilio wa mambo. Siamini. Ila naweka nadhiri kutoshirikiana nazo kamwe. Nimekula makavu tangu kitumbua chetu kilipoingia mchanga, mapenzi, utu, uaminifu, ilhamu ya kuishi, urazini, ela sitaki kupoteza heshima yangu. Mambo yangu tangu sasa nitayafanya mwenyewe bila kuchangiziwa. Hisia huchochea mtu akatenda mambo yasiyo murua mwisho akajiuma kidole, sitaki kujutia asilani. Natumai umezipokea salamu zangu. Salamu baridi ambazo kwa sasa zinanitoka tu ahlan wa sahlan. Sina rai. Si laiki yangu kukuamkia kwa ubaridi baridi hivi kana kwamba hatuhusiani kwa damu wala usaha. [Juzi tu tulikuwa tunaamkiana kwa pambaja za mahaba] Kumbuka huu ni mojawapo ya mikataba niliojiwekea. Kutoruhusu hisia zangu kuniongoza.
Mengi yamejiri baina yetu. Mazuri na mabaya, ya shani na shari ila zito kabisa ni hili la mfarakano wetu. Mfarakano ulioniachia ukiwa sina mhisani. Silaha ya pekee niliyo nayo ni machozi. Wazo la kutoswa ndilo linalousugua moyo kabisa. Hata ningejifariji kuwa nitakupenda hadi kifo, lazima nikubali kuwa mapenzi yanataka ridhaa ya pande zote mbili. Kung’ang’ania mapenzi kwa upande mmoja ni sawa na kusubiria embe chini ya mnazi. Nachelea kuwa hatukupiga hatua zozote katika safari hiyo tuliyokuwa tumedhamiria kusafiri bega kwa bega. Siamini. Tuliyoyapanga yalipeperushwa na upepo. Sasa zimesalia kumbukizi tu. Kumbukizi zinazochochea hisia na kuchukuwa hatua kufanya jambo. Kulipiza kisasi pengine. Kisasi? Mbona moyo utunge feli na kufanya njama dhidi yako ilhali ulikuwa faraja ya moyo wenyewe? Ama ndiyo yale ya kulipa mema kwa mabaya. Wewe ndiwe uliyekuwa tiba mujarabu ya donda langu la moyo. Waliosema husema kuwa ulikuwa nyongo mkalia ini. Siamini kabisa. Huenda hisia zangu zinapania kunichongea na kuniponza tena. Subiri nizidhibiti kwanza!
Saumu, natumai u mzima hadidi. Natarajia kuwa mawimbi ya ndoa yako hayajaufuta uzuri wako wa hurulaini ulioninasa kwa mnato wa gundi na kuyatia macho yangu nuru. Ni huo mnato wa uzuri wako ulionisadikisha kuwa mimi na wewe tulifaa kuwa pamoja na kuchangiana nasaba. Nikawa siwezi kuona mwengine badala yako. Na endapo nilijitia ukengeza, basi wema wako ulinifanya niwafumbie macho wengine wenye ari walionitaka usuhuba ila nikawakatalia mbali. Nitazifuta vipi kumbukumbu za enzi zile, ukiwa tunda bichi hujadokolewa. Ulikuwa watoka sokoni, nakumbuka fika nilivyokurushia ndoano ya huba. Nawe nadhani ulikuwa limbukeni kabisa katika bahari hii. Huna tajiriba wala ufahamu wake. Upo tu ufukweni, hujawahi kupiga hata mbizi kwa woga wa kutojua tamu na chungu ya nyonda. Muda ule ulikuwa hujadiriki kuchomeka walau kidole chako mzingani kuonja tamu ama shubiri ya nyonda. Ulivyokuwa unachorachora ramani kwenye mchanga kwa fazaha ukitumia dole gumba, uso umeuficha kwenye viganja vya mkono. Hujifai kwa izara na tahayuri. Nilitunga subira na kukufunulia kurasa za moyo wangu kuhusu hisia zangu kwako. Nikasoma kila ukurasa kwenye kitabu cha mapenzi yetu ili uelewe barabara nilivyokuwa nimesalitika kwako. Nami nikipania kuifukia mbegu ya mapenzi kwenye shamba lako licha ya sitaki-mama-kanionya-bado –nasoma zako. Mbali na upole wako, sura yako iliyokuwa na mvuto wa sumaku ilinivuta na kunivutia. Mbali na hayo, nasadiki na kuamini kuwa mbali na uzuri wako tabia zako nzuri ndizo zilizotia kitone na kuakifisha makisio yangu kuhusu ukamilifu wako. Nikakata shauri kuabiri nawe katika mtumbwi wa huba liwalo na liwe. Wajua tena tabia ni moja wapo ya nguzo mathubuti ya kulinganua uaminifu wa mja. Na yako haikuwa na dosari hata chembe.
Yalikuwa mapenzi ya kweli ama ulinifanyia usihiri? Siamini, huenda ulinipiga mzizi nami sikuwa na mwao kutokana na upofu wa nyonda zako. Nilivyotokea kukuenzi si kawaida yangu. Sijawahi kumpenda yeyote jinsi hiyo, nilipokudondokea, yangu na yako yakawa si ya siri tena bali ya dhahiri. Unakumbuka siku tuliyoshikwa na kusimamishwa mbele ya wanafunzi wote shuleni kwenye gwaride? Licha ya aibu iliyotupata sikulikatia tamaa penzi letu. Nilikuwa tayari kujitoa kafara kwa ajili yako Saumu. Na nisingekuwa wa kwanza kama watu walivyokuwa wakisema. Unakumbuka kisa cha Romeo na Juliet sio? Kumbe penye wema hapakosi wenye shari. Basi wenye joyo la mdimu wakasema ya kusema. Maneno yao yakaota mbawa na kupaa hadi yalipowafikia walimu. Walioyafikisha haikosi kuwa ni wale wanafunzi ambao daima walituonea gere. Ya kwao yalikuwa yamewashinda ndiposa wakaanza kuyanyemelea ya kwetu. Nao wakazuumu kulizima penzi letu kwa ukuti au mauti. Alikuwa anaitwa nani yule mwalimu? Simkumbuki uzuri. Bwana Mwakila Safari, aliyetufunza somo la dini. Nadhani alifaa zaidi kuwa jasusi hasa. Alivyounga moja na moja hadi akatuhumu na kushuku usuhuba wetu kimesalia kuwa kitendawili kwangu hadi leo. Alijuaje kuwa nilikuwa nikikuandikia matini ya Fizikia na Giografia? Ama kuna kidudumtu aliyekuwa akitulilia ngoa pasi na sisi kung’amua? Siamini kwamba ilikuwa bure. Lazima alikuwepo wa feli aliyetuendea kinyume. Binadamu lazima walijishengesha tu katika mambo yasiyo wahusu. Wakatwaa vya kutwaa na kuvigawa kwa faida ya mahasidi. Hukuamini kuwa niliyafanya hayo kwa dhati ya moyo?
Basi nikaadhibiwa kimotoni mpaka nusra nitoe ngama. Yote kwa sababu yako, ama bora niseme yetu kwa namna tulivyokuwa tumeshibana, jinsi penzi linavyopofusha! Nakumbuka nilivyosulubishwa kwa kupigwa na walimu takribani kumi na wanne. Nikatoka afisini natembea maga maga. Viboko vimeniota makalioni. Sikwambii vicheko na dhihaka zilizonilaki darasani. Bwana Olang’, naibu wa mwalimu mkuu, ndiye aliyekuwa mlungizi katika masuala ya nidhamu. Alipenda sana matukio kama hayo. Alivyotoka afisini mwake amekunja shati majasho yanamtoka nilifahamu wazi wazi kuwa ningekioana kilichomtoa kanga manyoya shingoni. Dua yoyote niliyokuwa nimeazimia kuitoa isingenifaa kwa lolote lile. Saumu, nilivumilia hayo yote kwa sababu ya penzi letu, nami niliamini kuwa uliona jinsi nilivyojitoa sadaka kufa kikondoo kwa manufaa ya penzi letu. Siamini kuwa hilo halikukupiga mshipa. Ningefanya nini kipya chini ya jua kukudhihirishia kuwa ni wewe tu ambaye ulikuwa umeuteka moyo wangu? Ulipoamua kuondoka hukuangalia nyuma tena. Machozi yalinipukutika siku hiyo kama kitoto kikembe kilichohiniwa ziwa na mama yake. Yalikuwa machozi yangu ya kwanza kunitoka kwa sababu ya mwanamke. Hata mama yangu mzazi sikumbuki ni mara ngapi nilikwisha dondosha chozi sababu yake, sikumbuki kamwe.
Watu waliowahi kuniona mosi zile haweshi kupigwa na bumbuazi jinsi nilivyobadilika. Nilikuwa sijifai. Siyaendeshi mambo yangu kama zamani. Nimeyaacha yaniendeshe yatakavyo. Nipo tu kama kivuli. Nafuata kiwiliwili maadamu alishautoa uhai uliokuwemo. Taathira ya mambo niliyopata kuyasikia na kuyaona kwa macho yangu ilikuwa imeniachia ulemavu moyoni. Moyo ukawa hauwezi kufanya kazi kama zamani, unahitaji mikongojo ujikongoje kwa dhiki na mateso ukikumbuka jinsi ulivyoutosa. Nikasota tangu ulipotengua kiota cha mapenzi nilichokuwa nimekijenga kwako. Kula nikawa sili, nikila ni kwa kushurutishwa tu. Usiku sikupata hata lepe la usingizi, nilalapo hunijia jinamizi nikapepesuka na kukesha na tasbihi vitangani navuta nyiradi, mara naghafilika najikuta nataja jina lako kati ya Subhanallah na Astaghfirullah. Huo sio usihiri? Siamini. Nimepoteza dira kabisa. Ari na ilhamu ya kuishi vimenyauka kabisa kama majani ya mto katika msimu wa kiangazi. Nipo tu, maadamu nachelea kuhalifu kanuni za Muumba kwa kujitia kitanzi. Siamini kama kifo ni suluhu mujarabu kama wanavyoamini watu wengi siku hizi. Japo kifo ni faradhi, huja kwa kudra wala hakifai kuja kama suluhisho wakati wa mtihani kama huu.
Kujitia kitanzi ujifilie mbali hakupunguzi wala kuzidisha lolote. Aidha, huwazidishia ugumu wafiwa mbali na kujikatia tiketi ya kuingia jahanamu moja kwa moja. Nachelea kumliza mamangu. Naogopa kumzika angali hai. Kila ninapomtupia jicho huhisi ana fundo moyoni. Kitendawili cha nani kamponza mwanawe kinamlewalewa machoni. Sitaki kumpasulia jipu lingali halijaiva. Haijuzu mtu kujitoa uhai. Nitakosa cha kusema mbele ya Mola tutakapokongama mbele ya haki ‘kwenye kivuli cha mkunazi’ chambilecho mwimbaji mmoja wa taarab, usuli wake pwani ya Kenya.
Habari za kuolewa kwako zilivumishwa kwa weledi. Unaelewa fika jinsi watu wa kwetu huku walivo magwiji katika kujishengesha katika mambo yasiyowahusu unywele ama wayo. Wamekubuhu. Wanashahada za uzamifu katika umbeya. Sisemi mabaraza na kamati zenye wanachama wa kudumu katika kusongoa mambo ya watu. Hatimaye baada ya kufanyiwa tafiti na uhariri wa kimataifa, zikanifikia. Kuna msemo maarufu sana kwamba umbea unahitaji bidii. Zaidi ya bidii hawa naamini kuwa wana talanta. Nadhani mdaku wangu aliyenibukulia habari hiyo alikuwa ameivalia njuga si kidogo. Alinieleza nini akasaza kipi?
Kwamba lodi mmoja amenipiga kumbo na kuninyang’anya tonge langu mdomoni halikuwa jambo la mjadala tena mtaani. Nilipodadisi nikaelezwa kwa ujana wake bwana yule wote amekulia Uarabuni. Amefanya kazi za mtulinga na za utumwa akaweka akiba sijui miaka ishirini na… Upo wakati kulizuka tetesi kuwa alikuwa ameuawa huko kwa kosa la kumbaka mtoto wa mwajiri wake. Wazazi wake hawakupata habari yoyote kutoka kwa mwana wao aliyehajiri kwa takribani nusu mwongo. Wakaamini kuwa Izraili alikuwa ametekeleza wajibu. Watu wa mji wao wakajaza madoo na madoo ya machozi kwa kumpoteza mwana. Uchungu wa mwana waliujua wao kuliko hata mama yake mzazi. Ndio maana ilipobidi waliuzika mgomba kama kanuni na desturi zao zinavyoeleza. Matambiko yakafanya kumleta mwana wao aliyejifia katika mateso huko mashariki ya kati.
Kisha ghafla bila taarifa akazuka kama mzuka. Wengi wakaamini ni mazingaombwe. Imani zilikuwa zimetikisika. Waliokuwa wamelia na kuomboleza wakaajabia na kuulani ujio wake. Alikuja kwa hadhi na uluwa. Hakuwa yule kijulanga mkondefu aliyetoka zamani kwenda kusaka tonge. Umbeja na umaridadi ulimwandama. Alikuwa mwenye afya na sauti. Sauti ya kusema na kutenda ilimtoka. Ngozi yake nyororo iliwasahaulisha makovu na nuksani zake za awali. Baadhi ya watu wakanong’ ona kuwa alikuwa kakoga maji ya zam zam. Alikuwa kachuma kwenye jua la Uarabuni naye karudi kijijini kulia kivulini kama inavyosema lulu ya wahenga. Hazikupita siku kadhaa ikawa dhahiri kuwa hakumiliki mashangingi tu bali alikuwa na mashamba, akiba ya pesa kwenye mabenki. Moja kwa moja, jina lake lilifutwa katika kijitabu cha wasio navyo pale kijijini na kuandikwa katika kitabu cha malodi waliokuwa wakipeperusha bendera ya utajiri. Dunia ni mapishano.
Nilizipokea habari za ndoa yako kama mgonjwa apokeavyo matokeo ya daktari ya kutamausha na kukatisha tamaa. Kwako na kwa wanakijiji wengi zilikuwa habari za kupendeza mno, habari za kupumbaza nafsi na kufariji. Vigelegele na riboribo vilipokezanwa na kuyeyushwa kwa vicheko.
Nakumbuka nkiwaskia watesi wangu wakigongeana bilauri na kurembua macho huku wakizingua ‘harusi tunayo ama hatuna?’ Nilikwaruzika sana. Ulimwengu ulikuwa umeungana kuniumbua. Ama ni mimi niliyekuwa nimekataa kujiunga na ulimwengu kukupa mkono wa tahania? Nao waliosema dunia mduara hawakukosea, niliyokuwa nikiyasikia yakazunguka hadi ya kuzunguka hatimaye yakanifikia. Ikawa zamu yangu ya kufaidi chungu wa nyonda. Lakini mbona mtu arambe chungu wakati tamu haijamkolea vizuri ulimini? Hatimaye, kengele za harusi zilipigwa na harusi kunadiwa. Tetesi zilizonifikia ni kuwa bwana harusi alifungua kibindo siku ya kwanza ya posa. Kisha baadaye akafumua mali kochokocho kama mahari. Sikuamini. Japo huenda hilo nisingelifanya, nahisi haikuwa sawa kwangu. Mbona hukuvumilia ili kesho tufaidi tamu ya subira yetu? Ama ulighairi nia baada ya kuona pangu pakavu?
Kosa langu hadi leo nimeshindwa kuling’amua. Ama ulitekwa na uluwa wa yule lodi? Uchochole ambao ulikuwa mirathi yangu kutoka kwa wazazi wangu haukuwa chaguo langu. Halikadhalika, najua hilo lilikutia hofu sana. Mwanamke yupi anayeweza kujiingiza katika mikatale ya ulofa katika karne hii? Gogo la mbuyu si la mvule Saumu. Na iwapo yupo basi ni mmoja katika elfu. Unamtafuta kama sindano kwenye shamba la mpunga. Hukuniamini kabisa nilipouma meno masomoni na kufuzu na kuingia katika chuo kikuu? Chuo cha umma! Zilikuwa juhudi za kukuwekea mustakabali mzuri. Hukuona? Hukuamini kuwa nilikuwa najituma kwa minajili ya kesho yetu pamoja? Kesho yenye uketo wenye hadhi na afadhali. Nawe ukaniacha bila heri wala kwaheri. Ukauacha mlango wazi mwenzio nadhani utarudi kumbe naipoteza sudi? Hukutaka kufa maji ukiuona ufuo. Siamini.
Basi ukaikata kabisa mizizi ya mapenzi iliyokuwa imeanza kuchanua na kutanda kwako. Ulinidhihaki, nikaungulika ndani kwa ndani, nikajikaza madhali muungwana hununa moyoni wala sio usoni. Lakini siku ya siku ilipofika sikuweza kujizuia. Machozi yalinitoka kapa kapa. Nikaamua kwenda kuuficha uso wangu kwenye kingo za mto Lumusu. Kule tulikozoea kwenda kutabaradi kabla ya mapenzi yetu kuanza kutifuliwa na mihemko ya pesa. Nikashinda huko nikiweweseka kama mtu aliyepagawa. Jioni hiyo chakula kilikosa ladha. Kichwa kiliniwanga nusra kipasuke. Nilipoibuka kutoka katika tukutiko hilo, moyo ulikuwa umetunga kutu na kufanya fundo. Fundo lililoufanya kuzizima na kuwa jangwa lisiloota hata mtende. Nakumbuka nudhumu niliyoitunga kama kumbukumbu ya dhoruba ulilonachia. Niruhusu nikudokolee japo machozi hunidondoka milizamumilizamu kila ninapofukua kumbukizi hizo.
Siamini ‘menitosa, mchangani bila kosa,
Hukusema langu kosa, mwengine keshakuposa,
Zimenitoka hamasa, kwa uno wako mkasa,
Nitaridhiya baghala, kwa kukukosa farasi,
Hukulithamini penzi, kipofu sikutambua,
Nisije fumbata konzi, wema nikauchubua,
Huba sasa kitenzi, mtegoni najikwamua,
Nitaridhiya baghala, kwa kukukosa farasi,
Mkufu nimeuvua, kukupenda sitamani,
lije jua ama mvua, nitashinda mtihani,
Mafuta kikosa jua, maji hupakwa mwilini,
Nitaridhiya baghala, kwa kukukosa farasi,
Yapo mengi ambayo ningependa kuyasema. Huenda nikautua mzigo mzito nilioubeba moyoni. Mengine naona bora niyahifadhi moyoni yagande na kukaukia mumo humo. Japo naelewa ni muhali sana moyo kufuta mambo, kidogo tu, na unayafufua yote na yakaendelea kuishi hadi siku ya kiama. Ndio maana naona bora yasalie katika hifadhi ya milele. Hifadhi ambayo haifikiki katu hata kwa ushawishi wa kijasusi.Kwa sababu katika kujaribu kuyatongoa najipata nikichubua kumbukumbu zenye uchungu usiovumilika. Na tujuavyo kuwa mwenye kovu haponi kabisa kabisa. Huhitaji kuchubua tu kidonda kidogo na bila shaka ataanza alifu kwa kijiti kujiuguza. Kuna mwimbaji mmoja aliwahi kusema kuwa penzi ni donda la moyo. Donda la kuuguzwa milele kwa kuwa kupona kwake ni muhali sana. Hata baada ya miaka na dayari, mwanadamu husalia na taadhari ya mapenzi, hasa iwapo yalikuwa ya dhati. Nimeamini kauli ya hayati mwanamziki huyo. Aliyoyasema yamejisadifu kwangu. Nimepanga na kupangua. Nimewaza na kuwazua. Nimeishi hadi sasa naishiwa. Katika kujaribu kujifunza machache, nimegundua mengi. Katika mengi niliyoyagundua nimejifunza machache; kutoamini wanaotaka kuaminiwa. Kweli siamini.
WRITER – JIBRIL ADAM
