Moyo hupata tuliya, furaha tele moyoni
Kila ninaposikiya, na kukuona machoni
Uelewe hili piya , kinitazama usoni
Subira nasubiriya, kujua yako maoni

Kwako moyo umetua, nimeshindwa kulisema
Sijui kama wajua , tangu siku za mapema
Moyo ulikuchagua, kwa tabia zako njema
Ni wakati kuamua, sikiza wako mtima

Nami mwangu mtimani, nitapata kuridhia
Wewe ‘kiwa wangu hani, Mola akijaalia
Kheri njema maishani, kwa Mola twatarajia
Huba liwe la amani, upendo wa familia

Haya yote fikiria , ninasema si utani
Nitaweza vumilia, kama uko na mwendani
Pia moyo tatulia, kama maji mtungini
Sasa nataka sikia, moyonimo mna nani?

Fanya hima kunijibu, mapema nipate jua
Pia sione aibu, kama ninakusumbua
Fikiri kwa taratibu, mafumbo kuyafumbua
Tabaki kuwa sahibu, ukweli nikitambua

Masomo siache kando, ukaumiza kifua
Kwa sababu langu pendo, awali hukulijua
Endelea mbele mwendo, hadi mwisho wa hatua
Katu penzi siwe fundo, ukashindwa kutatua

Mwanzo upange mipango, ya masomo na maisha
Utimize lako lengo, kila kitu hakikisha
Usiache hata pengo, au mambo kusitisha
Basi soma hizi tungo, ujumbe nimefikisha

Alhamdan Mohamed
Kalamu Dumu Daima
Mombasa

WRITER – HAMDHAN MOHAMED

Categorized in: