Kupenda sana hatari, neno hili nawambia
Penzi ni kama bahari, mawimbi huyumba pia
Nawapa hii habari, mupate kufikiria
Chunga usisidimie, majuto ukajutia

Ogelea kwa hadhari, kwenu hili nahimiza
Tena ukitafakari, hutoweza kuteleza
Kuna wema pia shari, haya yote peleleza
Chunga usiangamie, au kumezwa na pweza

Walojipiga vidari, wako wapi nambieni ?
Yamewakuta tayari, madhila mwao nyoyoni
Wale walo mahodari, leo wamo matatani
Chunga usilivamie, penzi halina utani

Muombe Mola Kahari, uwe bora baharia
Akupe nyingi bashari, akufungulie ndia
Ndoa ni bora safari, chombo hicho shikilia
Chunga usikimbilie, baharini kuingia

Alhamdan Mohamed
Kalamu Dumu Daima

WRITER – HAMDHAN MOHAMED

Categorized in: