Nini kinakusumbua, dhambini ukajitia
unafanya ukijua, kuwa hiyo ni hatia
Ni vyema ukaradua, kwa Ilahii kutubia
kwanini hujaamua, maasi kuyakimbia
Ninini kinakughuri, ukasahau ya kheri
Hivi hunayo habari, kuhusu ile safari
Hebu ifunge dhamiri, kuyaandama mazuri
usichanganye uturi, na uchafu wa kiburi
Tazama wanadondoka, waloishi kwa kutamba
Tazama wanatoweka, wanene pia wembamba
Bado hatujazinduka, twaasi tukijigamba
Hebu tubia hakika, Rudi Sasa kwa Muumba
WRITER – ALI HILAL