Ewe mfuma mipango, kwangu iso mipendezi

Ulokithiri urongo, na sifa za kijambazi

Nakufikisha ukingo, kwangu hutopiga mbizi

Ngoma yako siichezi!

 

Siichezi Maimuna, ungahamu niwe mumo

Kuihiari hakuna,katu sitokuwa chumo

Kwangu huna la kuvuna, nimeshajifunza somo

Ngoma yako siichezi!

 

Uwanja wako telezi, sinao imani tena

Utakalo siliwezi, hatunao muamana

Yakomeshe maigizi, mwana mja wa laana

Ngoma yako siichezi!

 

Ni michochezi midundo, unayoniandalia

Ila ni yenye uvundo, ninavyoikadiria

Itanizulia fundo, kesho nikajajutia

Ngoma yako siichezi!

 

Sinayo hamu sinayo, ya kuuguza makovu

Nina kimoja kijoyo, kisotindikiwa wivu

Na kwa hayo nionayo, najitanibu na nyavu

Ngoma yako siichezi!

 

Sishiriki ngoma yako, yenye washirika wengi

Ikanipa hamaniko, mja niso na shilingi

Bora nikae kitako, nijiepushie mengi

Ngoma yako siichezi!

 

Mtunzi: Jibril Adam 

Lakabu: Malenga wa Jangwani. (Abu Sanaya)

Nairobi Kenya.

WRITER – JIBRIL ADAM

Categorized in: