INAVUNJA MOYO kwamba wakati huu ambapo wanafunzi wa shule za upili wanapoendelea kufanya mitihani yao ya kitaifa, visa vya udanganyifu vinavyoripotiwa vinawahusisha walimu. Waziri wa elimu amenukuliwa akitaja kuwa walimu wamehusika kwa njia moja ama nyingine katika uhalifu huo. Walimu ni wataalamu wenye heshima kubwa katika jamii. Wana jukumu zito la kuhakikisha kwamba wanakuza maadili ya wanafunzi watahiniwa wanaofanya mtihani kwa sasa ili siku zijazo waweze kuwa tegemeo la nchi yetu. Visa vya walimu kula njama na wanafunzi wahalifu vinadhihirisha uozo, kutowajibika,ukosefu wa uzalendo na hata kukuza uhalifu usiokubalika kamwe.

Maswali yanayoibuka kuhusu hulka hii ni mengi. Yawezekana walimu wanashawishika kuwapiga jeki wanafunzi kutokana na matayarisho duni? Ama kuna misukumo ya ndani kwa ndani? Dhima ya walimu ni gani hasa?

Serikali na taasisi husika hazifai kuyafumbia macho matukio kama haya. Huenda yakaleta maafa makubwa baadaye. Wazazi wana jukumu la kuwaadilisha wana wao kwa maneno na vitendo, vinginevyo tutajipalia makaa.

Jibril Adam Nairobi, Kenya.

WRITER – JIBRIL ADAM

Categorized in: