Mwandishi Ibrahim Hussein, kupitia mhusika Kinjeketile katika tamthilia yake ajwadi yenye jina lilo hilo ‘Kinjeketile’ anasema kuwa, binadamu huzaa neno-neno hushika nguvu-likawa kubwa-kubwa, kubwa likamshinda binadamu kwa ukubwa na nguvu. Likamwangusha. Je, ni kweli kuwa neno ambalo limezaliwa na ntu laweza likaja kuntawala ntu yule yule aliyelizaa? Katika msimu huu wa uchaguzi, nchi imeshiba joto la kisiasa na sasa inaliteuka katika kila pembe. Kila mwanasiasa (na hata wasiokuwa wanasiasa) wamejitosa uwanjani kuwania nyadhifa anuwai. Wanasiasa hawa wapandapo kwenye majukwaa, wanaonyesha ufundi wao katika kuwashawishi wapiga kura ambao ndio hadhira lengwa. Kuna kichekesho maarufu kinachotamba vijiweni kuwa ukirusha jiwe kwa bahati mbaya, kuna uwezekano mkubwa likampata mgombea ubunge ama mwakilishi wa wodi. Yakini, kwa sasa simu za waheshimiwa zinafanya kazi. Hazijazimwa kama zilivyokuwa hapo awali. Kwa sasa wanapatikana kwa urahisi. Sitaki kutaja kwa mapana kuhusu unyenyekevu na upole tunaoshuhudia kutoka kwao. Hata wale ambao walikuwa wameadimika kama wali wa daku wamejitokeza na kuanza kupitapita machoni mwa wapiga kura. Yote haya wanayafanya kama njia ya kuwarai tena wapiga kura kuwapa nafasi za kuingia madarakani ama kusalia kwenye nyadhifa za uongozi kwa masilahi yao wenyewe. Waliosema kuwa mwomba chumvi huombea chunguche hawakusibu. Jambo linalonipiga mshipa niandikapo makala haya ni kauli zinazowatoka wanasiasa hawa wanapojikalifu juu chini kuwapa wapiga kura nyama ya ulimi. Si mara moja, utawasikia wakihemkwa huku wakitoa ahadi tele kama mchanga wa bahari pamoja na kauli zinazoweza kuhatarisha usalama na mshikamano wa taifa. Ukizipiga darubini ahadi na semi zenyewe, utashindwa kuelewa iwapo ni ahadi za Kiswahili ama ni ahadi zenye chembe ya ukweli. Pana haja ya taasisi za kuchunguza na kudhibiti kauli chonganishi kama hizi kuwajibika kikamilifu. Baadhi ya kauli kama vile ‘madoadoa’ ‘watu wetu’ ‘kila mtu arudi kwao’ hazipaswi kuvumiliwa si wakati huu wa uchaguzi tu lakini hata wakati wowote ule hapa nchini. Kauli kama hizi zinatishia kuitosa nchi katika kinamasi cha mapigano yanayochochewa kwa misingi ya kisiasa kama yale yaliyoshuhudiwa katika chaguzi za miaka ya hapo awali, hususan 2007. Waama, mwenye kovu usidhani kapoa. Ni matumaini yangu kuwa wanasiasa watajirudi wenyewe wanapoendeleza harakati zao za kutafuta uungwaji mkono na kutaka kuteuliwa katika nyadhifa tofauti. Suala la kuteuliwa lisiwe la kufa kupona. Amani na maridhiano vipewe kipau mbele kuliko tamaa za watu binafsi. Vile vile, ni wajibu wa kila mwananchi mzalendo kupambanua mbivu na mbichi. Asiwe bendera ya kufuata upepo, si shimali si yamini bila kujua ngoma inachezwa kwa miondoko gani. Shime wananchi wanaotahadhari, ama kweli, mjenga nchi ni mwananchi na mvunja nchi ni mwananchi. Tusifurutu ada na maadili kwa utovu wa sheria kisha tukaalika hasara na madhara makubwa kwa maneno ya vinywa vyetu wenyewe. Mwandishi wa makala. Adamu Jibril Abu Sanaya.
BY JIBRIL ADAM- Writer
