Kwa isimu yako Mungu ,nudhumu naikadimu
Napiga magoti yangu ,nisifu na kuheshimu
Macho nelekeza mbingu, anga nikiizuhumu
Tuokoe tunakufa ,gumba imetuandama.
Ewe uliye Maliki, mmiliki kila kitu
Pekee unastahiki, kupokea sifa zetu
Tuepushie na dhiki, ilotushukia kwetu
Tuokoe tunakufa, mahuluku na bahimu.
Nikitazama suheli, taabu ni ileile
Anga imetulia tuli, mithili ya maji male
Imenibidi nikuli, nikiwa huku Kitale
Tuokoe tunakufa, mimea imenyauka.
Hakika linatudhili, shamsi tukitazama
Jua limetutia feli,launguza likichoma
Usipobadili hali, dunia tutaihama
Tuokoe tunakufa ,hatuendi tunasota.
Ya ilahi ya raufu ,Mungu mwenye upole
Wewe ulo ashirafu, dua yangu usikile
Tupe mvua latifu ,tufurahi kama kale
Tuokoe tunakufa, gumba imetuandama.
Moses Chesire
Sumu ya Waridi
Kitale
WRITER – MOSES
