(Ushindi Wa Pawa 2021 Baada Ya Orodha Fupi Ya Mabati-cornell 2018)

Alhamdulillaah alaa kulli haal! Nahmaduhu wanuswallii alaa rasuulihi-l-kariim!

“Sijawa ni nguli, mbele ya wajuzi” “Bado niko mbali, kukana siwezi”

Kitendo cha diwani yangu ya Wino wa Dhahabu kutangazwa kama diwani bora ya Kiswahili katika Tuzo ya Ushairi ya Afrika inayoendeshwa na kusimamia na taasisi ya Pan-African Writers Association (PAWA), kimezidi kunifundisha na kuniongezea mambo mawili makubwa:

  1. Kupata Kuna Jalali kama nilivyowahi kuandika katika moja ya shairi langu, mnamo mwaka 2018.

Nakumbuka wakati tangazo la tuzo hii likinifikia kupitia ukumbi wa kundi sogozi la WhatsApp liitwalo MALENGA CHIPUKIZI, siku ya terehe 06.10.2021 saa moja asubuhi huku zikiwa zimebaki takriban siku ishirini na tano (25) dirisha la kupokea mawasilisho ya kazi kwa washiriki kufungwa. Na wakati naandika andiko hili, nimemuona hadi aliyelileta tangazo hili ukumbini, Dada Fatma Ali Mohamed wa Wete, kisiwani Pemba (Mola Amhifadhi). Sikusita wala kupata gagaziko kuwa natakiwa kushiriki. Siku nne baadaye, sawa na tarehe 10.10.2021, niliamua kushiriki kwa kutuma baruapepe yenye nakala tepe za diwani yangu (jalada na kurasa za ndani) kama tangazo lilivyoelekeza.

Mbali na kushiriki kwangu, sikuona uzito kuwashajiisha na wenzangu ambao katika vigezo niliamini wanakidhi akiwemo kakangu Ali Mohamed (Kilio cha Sisimizi) na walillaahil-hamd naye aliingia katika orodha fupi kwa diwani yake niipendayo, diwani ambayo katika hatua za uhariri wake, ilipita mikononi mwangu. Lakini, kushika nambari moja hakuna maana kuwa mie ni nguli zaidi yao, bali ndiyo twarejea palepale “Kupata Kuna Jalali”

  1. Uchu na shauku ya kuzidi kuandika na kuwahamasisha washairi waandike na kuchapisha kazi zao

Nilichogundua ni kuwa kuna wingi wa kazi za ushairi kutoka kwa washairi mbalimbali lakini kuna uhaba mkubwa wa kazi za ushairi wa Kiswahili ambazo zimeshachapishwa. Miongoni mwa vigezo vya tuzo hii, kimoja kilikuwa ni kuwa; kazi ambayo itawasilishwa iwe imeshachapishwa katika ya mwaka 2018 na 2021. Na bila kupindisha kauli, kazi za Kiswahili zilizowasilishwa zilikuwa ni 8 kati ya kazi 363. huku lugha ya Kiarabu ikipokea vitabu 88, Kingereza 179 na Kifaransa 88. Unaweza ukaona namna ambavyo kazi za Kiswahili zilikuwa chache. Japo hii inaweza kuwa imechangiwa na kuwa ni mara ya kwanza kuitisha kazi za Kiswahili.

Kutokana na hali hii, nachukua fursa ya kujituma niandike kazi nyingi zilizo bora, na kuwahamasisha wenzangu kuchapisha kazi zao kwani licha ya kuwa soko haliridhishi sana lakini kuna faida nyingi za kuchapisha mbali na dhamira kuu ya kuwazawadia watu fursa ya kusoma fikra zao.

Nimalizie kwa kunukuu beti zote kumi (10) zilizounda utungo wa “Nakupenda”. Utungo ambao unapatikana katika kurasa nambari 144-146 ndani ya diwani ya Wino wa Dhahabu;

Nyonda wangu, usozeeka dahari

Huba langu, juu yako ni kabiri

Roho yangu, ni wewe ewe kimwari

Usijeamba kwaheri ‘Taniuwa

Macho yangu, hayaoni yako shari

Kwona kwangu, inipendeze sayari

Dira yangu, i kwako ninakariri

‘Sitakalamu kwaheri ‘Taniuwa

Uso wangu, bashashale ladhihiri

Keti kwangu, penzi liwe ng’aring’ari

Ewe wangu, damuni wanishamiri

Usijenena kwaheri ‘Taniuwa

Pua yangu, ndiwe yakwita itiri

Moyo wangu, wakusadiki johari Chanda changu, pete nivaa vizuri Usijekuli kwaheri ‘Taniuwa

Figo langu, nitakupa e kigori Uwe wangu, katu usijeabiri Peke yangu, unipe penzi mahiri Usijesema kwaheri ‘Taniuwa

Hali yangu, pasi wewe sio shwari Cheko langu, washika moja nambari Mwenza wangu, ‘sifanye nitahayari Usijelonga kwaheri ‘Taniuwa

Bongo langu, kwako si tena jabari Pozo kwangu, nivishe umasururi Ewe wangu, n’nje wasijekughuri Usitamke kwaheri ‘Taniuwa

Dumu kwangu, hayati uiathiri Nipa vyangu, vya kwako kichinchiri Kulla changu, ki’ ndanimwo Al Huri ‘Kizungumza kwaheri ‘Taniuwa

Palo pangu, tuli awali akhiri Kuwa wangu, nife nawe kwa fahari Onyo langu, ukatili jihadhari ‘Sijepayuka kwaheri ‘Taniuwa

Mwisho wangu, si mwisho wa kuhadhiri Nuru yangu, nakusifu kwa urari Neno langu, “nakupenda ushairi” Usinutuki kwaheri ‘Taniuwa

Wito: Kila ajinasibishaye na uandishi, basi hatakiwi kuiacha kila fursa iliyopo mbele yake aidha iwe kwa kudhani kuwa yu mchanga au vinginevyo.

Pichani: Bashiru Abdallah (aliyevaa kanzu) akiwa na Ali Mohammed ambaye ndiye mwandishi wa diwani ya Kilio cha Sisimizi. Picha hii ilipigwa mnamo tarehe 30 Julai 2021 nje ya Mahakama Kuu ya Zanzibar, Vuga.


Abuw Haytham, Bashiru Abdallah Magole, Dar es salaam, Tanganyika. Jumapili, 10/08/1443, 13/03/2022

WRITER – Bashiru Abdallah

Categorized in: