Utafiti nimechuja, natoa mapendekezo,
Wa’jiri na mameneja, nimechambua mawazo,
Fukara nao na hoja, sijaacha mabakizo,
Vinywa vyao vimejaa, huyu adui tamaa.

Asilimia tisini, majibu yameshangaza,
Wako tayari kuhini, ili mali kuyajaza,
Hata kufuga majini, wamekuwa wakiwaza,
Vinywa vyao vimejaa, huyu adui tamaa.

Wapo wazi wamekiri, kuwa wa’budu sanamu,
Walitaka utajiri, kabidi watoe damu,
Wasema sasa ni shwari, katu hawajilaumu,
Vinywa vyao vimejaa, huyu adui tamaa.

Watu wamenishitua, kwa njama waliyopanga,
Walishiriki kuua, mali waipige chenga,
Hawakunifichulia, wasije kumwaga unga,
Vinywa vyao vimejaa, huyu adui tamaa.

Nilizidi kusaili, kwa nini kubwa tamaa,
Mmoja kanipa swali, la balagha nakwambia,
Kumbe waja mekubali, tamaa kutawalia?
Vinywa vyao vimejaa, huyu adui tamaa.

Tamaa ya makasiri, mavazi hela na nyumba,
Kwa wote ilishamiri, ikafwata ya mashamba,
Nyingine ni ya magari, ya rangi inayopamba,
Vinywa vyao vimejaa, huyu adui tamaa.

Asilimia kumi, ile iliyobakia,
Ilikuwa haisemi, waziwazi ukajua,
Ila kwazo zake ndimi, ungej’onea tamaa,
Vinywa vyao vimejaa, huyu adui tamaa.

Na sasa nimebaini, kumbe waja si wabaya,
Ni wazuri mtimani, ila tamaa yapwaya,
Si makosa kutamani, japo dhambi kuzidiya,
Kuishi maisha mema, insi punguza tamaa.

Allan Lumunyasi Chevukwavi.
Mwoshashombo.
Nairobi.

WRITER – ALLAN CHEVUKWAVI

Categorized in: