Dunia bahari chafu, siogelee kwa pupa
Itakukata mapafu, ubaki watapatapa
Tazama siwe kipofu, au kubaki mifupa
Imezoa wengi wafu, hutoweza kuichupa

Dunia mti mkavu, siagame binadamu
Utapata ulemavu, kukauka yako damu
Dunia hukata mbavu, hili nalo lifahamu
Dunia ni kama nyavu, jihadhari silaumu

Dunia ni mduara, kotekote umetanda
Huwateka watu nyara, mtego wa njia panda
Andika kwenye shajara, ili sipate kuganda
Rafiki acha papara, dunia sio kitanda

Kalamu Dumu Daima
Alhamdan Mohamed

WRITER – HAMDHAN MOHAMED

Categorized in: