Jicho lia mwaga chozi,nikomesheze udhia
Lia mwaga michirizi,ngawa kumi njianjia
Mwaga chozi langu ozi,mwaga nitakufutia
Kwani mwenzio siwezi,siwezi kuvumilia
Lia hata mbalamwezi,nisiione sawia
Lia mliwa mlizi,lia basi nakwambia
Hasira zangu mkizi,mvuvi kajivunia
Kwani mwenzio,siwezi na hilo wewe wajua
Japo kulia ni kazi,yahitaji mazoea
Lia utoe mauzi,na kila la kujutia
Lia kalamu nyerezi,
najua wanisikia
Kwani mwenzio siwezi,jengine ila kulia
Najua wajua wazi,mtima uhalisia
Sababu ni yule mwizi,chombo aloniibia
Mtwaa wa wangu mwezi,anga ulonangazia
Kwani mwenzio siwezi,kisha akautukua
Rashid Mwaguni.
Mombasa.
