Machozi yananitoka, kwa niliyosimuliwa
Yazidi nibubujika, ni vipi yatazuiwa? Yameniliza hakika, huzuni nimeingiwa
Kafanya hatia gani, huruma hukumwoneya?

Habari ‘lonifikiya, ni za yule hayawani
Kwa fujo zimeeneya, barani na hadi pwani
Kipi alichokoseya, mwana yule masikini?
Kafanya hatia gani, huruma hukumwoneya?

Njoo nawe twende huku, kwanza kumtamkiya
Nitakunulia kuku, na vibanzi kwa bajiya
Nikuletee mabuku, upate kujisomeya
Kafanya hatia gani, huruma hukumwoneya?

Mwana nae kakufwata, akawa ‘nafurahiya
Mkono hakukuwata, ahadi imemwingiya
Akavaa patapata, huyo akakufwatiya
Kafanya hatia gani, huruma hukumwoneya?

Vipi alikuvutiya, eleza nipate juwa
Hakuweza kuongeya, na wala hakukimbiya
Ukafanya kumwoneya, na haya hukuingiwa?
Kafanya hatia gani, huruma hukumwoneya?

Akalia “naumiya!”, hili hukulisikiya?
Ama nta ulitiya, kinyume ukamwendeya?
Wala si ajnabiya, ni mjomba wake piya
Kafanya hatia gani, huruma hukumwoneya?

Nywele zilimtimka, kichwani kumueleya
Nyute nazo kumtoka, machozi kumwagikiya
Roho ikamkatika, mbinguni ikapepeya
Kafanya hatia gani, huruma hukumwoneya?

Miguvu ulitumiya, damu tele kueneya
Yule mwana kajifiya,na wala hukujutiya
Sababu kujipatiya, madhara umeshatiya!
Kafanya hatia gani, huruma hukumwoneya?

Unadhani mtaani, huruma utaonewa?
Kama tadinu tudani, hilo kaa ukijuwa!
‘Lijifanya hayawani, sasa wadharauliwa!
Kafanya hatia gani, huruma hukumwoneya?

Subiri kuhukumiwa, chuma chako ki motoni
Utakuja kuvamiwa, kama nzige mhindini
Gerezani ‘sipotiwa, ‘tajipata kaburini!
Kafanya hatia gani, huruma hukumwoneya?

Ya ilahi tusitiri, tulinde na kila shari
Utupe na ujasiri, kutenda yaliyo kheri
Wana wetu wasitiri, dua kwako nakariri
Tuongoze ya Qahari, utupe yalo mazuri.

Alyah Kassim
Lulu na Marijani

Categorized in: