Umekatika wakati, kwa kuuotesha miye
Kwenye uwa katikati, tena niuhudumiye
Nikiiomba bahati, ukuwe nifaidiye
Sikupenda niumiye, kishapeya wangu mti
Huduma zangu za dhati, libidi niupatiye
Ili usifike kati, uhai uuishiye
Ona leo umeketi, siyaoni matundaye
Vipi uninyaukiye, nijilaumu mwanati
Ni kwanini tasliti, bwanawe unifanyiye
Na unajuwa thabiti, niliteseka juuye
Tena sana si katiti, vipi haya malipoye?
Siione hurumaye, nimebaki yalaiti
Bora ningejidhibiti, mateso nisijitiye
Ningekuwa salamati, tena bila dhahiriye
Nisingezipanga beti, waja niwahadithiye
Lakini kwa ajiliye, nimeshindwa kusukuti
Sasa nifike tamati, kinywa changu kinyamaye
Nimuombe Jabaruti, Pweke anihukumiye
Kwake nipige magoti, kisha nimsujudiye
Badali anigaiye, cha kunipa farhati
Abuw Haytham, Bashiru Abdallah
Magole, Dar es salaam – Tanganyika
Jumanne, 07/07/1443, 08/02/2022
