Sili kilofunuliwa, chakula hicho haramu,

Kisichofunikwa kawa, kwangu hakina utamu,

Msambe huku kulewa, nina akili timamu,

Sili kisichofunikwa, waandazi mtambue.

 

Wazi chakula kikiwa, wadudu hukihujumu,

Na tena hukichafuwa, pamwe na kutia sumu,

Maradhi nitauguwa, hasa kile cha karamu,

Sili kisichofunikwa, waandazi mtambue.

 

Kiwe mithili ngekewa, kuacha sijilaumu,

Hicho kimeshaingiwa, na nzi zamu kwa zamu,

Pengine kimechezewa, na wengi binaadamu            

Sili kisichofunikwa, waandazi mtambue.

 

Sili na haitakuwa, hata ikiwa ni nyamu,

Kiwe kimechapuliwa, hakinitii hanjamu,

Kula kisohifadhiwa, sawa na kujidhulumu,

Sili kisichofunikwa, waandazi mtambue.

 

Wala sijapungukiwa, kuhisi ladha ya ndimu

Na utamu wa haluwa, naujuwa mufahamu,

Siseme nasumbuliwa, umenipanda wazimu,

Sili kisichofunikwa, waandazi mtambue

 

Bure msijebukuwa, vitabu vya twalasimu,

Mkazimaliza duwa, ramli za kinajimu,

Sili nimeshaamuwa, hadi nende kwa Rahimu

Sili kisichofunikwa, waandazi mtambue.

 

Tamati mkielewa, ufanyeni ukarimu,

Wajibu kupambanuwa, maneno haya adhimu,

Vyakula kunadhifiwa, na kufunika jukumu,

Sili kisichofunikwa, waandazi mtambue.

 

WRITER – OTHMAN HAMZA

 

Categorized in: