Nihongwe mali muluki, ili kwako kubanduka
Sibanduki sibanduki, nimeganda muhibaka
Mwenginewe simtaki, hata angalinitaka
Nimeganda sitang’oka.
Au mafedha malaki, na ziara Amerika
Bado tasema sitaki, sikutaka sitataka
Hakuna hawakufiki, sioni wa kukufika
Bi maàna sitang’oka.
Nataka unisadiki, wala usitie shaka
Nafahamu hawataki, huba lilivyosimika
Wana chuki wana chuki, watuanapo twateka
Tua moyo sitang’oka.
Na sing’oki na sing’oki, hilo kichwani andika
Hata yangalidiriki, mauko yangu kufika
Nitakuganda ki ki ki, kama mpini na shoka
Sishopoki sitang’oka.
Sichomoki sishopoki, kuchomoka nikatoka
Iwe raha iwe dhiki, niko radhi kudhikika
Ng’oo! mi kwako sitoki, watanyoa watasuka
Sitang’oka sitang’oka.
Wanasema ”mtaliki, muache mpe talaka”
Ni vile hawakumbuki, kule sie tulotoka
Nitakupenda sichoki, watakonda watachoka
Watangoja sitang’oka.
Walete yao mikikiki, na vibaka kuniteka
Waende wakijinaki, watutusi na kufoka
Mie kwako nitasaki, na sini sita sinuka
Tasakini sitang’oka.
Wambie alamsiki, wakeshe na kuamka
Wakaze kila kasiki, watoe kafara paka
Mimi imara kisiki, sitang’oka kwa sadaka
Usijali sitang’oka.
Rashid Mwaguni
RMM
WRITER – RASHID
