Mwanangu njoo karibu, uketi unisikize
Nifanye wangu wajibu, ya dunia nikueleze ‘Tayasema taratibu, ili nisikutatize
Na wala usinijibu, kwanza ngoja nimalize
Kwa ulimwengu wa sasa , umaskini ni uvundo
Mwanangu nyakati hizi, imani hakuna tena Zilikwisha zetu enzi, za wingi kutetezana
Kwa alokuwa na kazi, kumjali aso hana
Ndipo likazidi penzi, na sisi tukapendana
Kwa ulimwengu wa sasa, umaskini ni uvundo
Waja wamebadilika, zimezorota tabia
Aila zimevunjika, urafiki nao pia
Na hapa tulipofika, utesi umechachia
Mengi yameharibika, na tumepotea njia
Kwa ulimwengu wa sasa, umaskini ni uvundo
Ukiwa ni mwenye chako, tajiri wa nyingi mali
Ni kubwa nafasi yako, wajiweza kila hali Utapata babaiko, watu wote ‘takujali
Lolote lako tamko, litafatwa kwelikweli
Kwa ulimwengu wa sasa, umaskini ni uvundo
Uwe na mbaya tabiya, na sura za kutishia Mabezo umejaziya, na kiburi kujitia
Na licha ya yote haya, kwa waja utavutia Hawatoona ubaya, bali watakukusifia
Kwa ulimwengu wa sasa, umaskini ni uvundo
Ukiwa ni masikini, kisha mbaya yako hali
Pato lako ni la chini, kujikimu ni muhali Hutoiona hisani, katu hawatakujali
La zaidi insani, watakukimbia mbali
Kwa ulimwengu wa sasa, umaskini ni uvundo
Hata uwe na huluka, nzuri iso kifani
Heshima ya kusifika, hutukani asilani
Waja watakuepuka,wakutoe akilini
Kwao ‘tasahaulika, ‘siulizwe abadani
Kwa ulimwengu wa sasa, umaskini ni uvundo
Nashika sikio lako, nakupa wangu wasiya
Katika maisha yako, siige hizi tabiya
Shukuru kwa hali yako, uzidi kunyenyekeya Usifanye babaiko, kwa mambo ‘soyafikiya
Kwa ulimwengu wa sasa, umaskini ni uvundo
Uwapende watu wote, fukara au tajiri
Silemee kwa yeyote, wala siwe na kiburi
Tabia zisizorote, ukija kuwa tajiri
Msaidie yeyote, katu usijifakhiri
Kwa ulimwengu wa sasa, umaskini ni uvundo.
