Mwenyezi wetu Rahimu, muumbi wa ulimwengu,

Mwenye sifa tamu tamu, uishiye kwenye mbingu,

Siku kitoa hukumu, na’mba situpige rungu,

Kenya siku ya kiama, tupewe adhabu ndogo.

 

Tayari tupo kuzimu, kwa hali tunayoishi,

Mambo yote ni magumu, ni kama tupo mazishi,

Situtupe jehanamu, tumeshauona moshi,

Kenya siku ya kiama, tupewe adhabu ndogo.

 

Tupo kwenye udhalimu, miili tumechupuka,

Tumelishwa hadi sumu, na wenzetu matajika,

Twatembea marehemu, twangoja wa kutuzika,

Kenya siku ya kiama, tupewe adhabu ndogo.

 

Tusifanye kazi ngumu, tayari tumeumia,

Tumenyonywa yetu damu, magofu tumebakia,

Ikifika hiyo zamu, tusikilize Jalia,

Kenya siku ya kiama, tupewe adhabu ndogo.

 

Utwonyeshe ukarimu, motoni usitutupe,

Wewe wa haki hakimu, utuoshe hili tope,

Pengine ikilazimu, tupigie tu utepe,

Kenya siku ya kiama, tupewe adhabu ndogo.

 

Mbeleyo tutasalimu, utufanye upendavyo,

Lakini jambo muhimu, usitupe vichoshavyo,

Natua yangu kalamu, kwa maombi niombavyo,

Kenya siku ya kiama, tupewe adhabu ndogo.

 

Allan Lumunyasi Chevukwavi.

Mwoshashombo.

Nairobi.

WRITER – ALLAN CHEVUKWAVI

Categorized in: