Maishani nalemewa, uzazi kulazimiwa,
Unyama nilitendewa, hadi mimba nikatiwa,
Sasa ni muathiriwa, mwili nilishahiniwa,
Kipi kwangu uliona, baba ukaninajisi?
Siku hiyo sikujuwa, mtego nikategewa,
Na baba nikaambiwa, mvungu kuinamiwa,
Punde hapo kafikiwa, mwana nikadhulumiwa,
Kipi kwangu uliona, baba ukaninajisi?
Maisha nilitishiwa, siri nisije fichuwa,
Kasema angeniuwa, watu watapombuwa,
Ila leo naamuwa, kuyatowa ya kifuwa,
Kipi kwangu uliona, baba ukaninajisi?
Tangu hapo kuzaliwa, ulikuwa mwaminiwa,
Hukuwahi fikiriwa, nguo ungenifunuwa,
Bintiyo nimeshajuwa, ya kumbe mtu hukuwa,
Kipi kwangu uliona, baba ukaninajisi?
Masomo nimekatiwa, na walimu nachukiwa,
Matusi ninarushiwa, afiriti nimekuwa,
Vipi hili liwe sawa, maswali yanibanguwa,
Kipi kwangu uliona, baba ukaninajisi?
Ndwele isiyotibiwa, mwilini nimeingiwa,
Siha nimeondokewa, kukicha nameza dawa,
Kiukweli naonewa, na kwingi kubaguliwa,
Kipi kwangu uliona, baba ukaninajisi?
Karibuni tafikiwa, uhai kukatikiwa,
Mtangani tafukiwa, kwa huko kuhujumiwa,
Mtoto nimeonewa, utu wangu kuvuliwa
Kipi kwangu uliona, baba ukaninajisi?
Allan Lumunyasi Chevukwavi (Mwoshashombo),
Nairobi – Kenya
