Magwiji na wenye ari , naja kwenu taratibu
Watunzi na wahariri, wa maneno ya dhahabu
Wasomi wa mashairi, mnipatie jawabu
Naja kwenu bila siri, kwa upole na adabu
Moyoni nina maswali, nataka kuwauliza
Nikianza la awali, nani atanisikiza ?
Lisiwe jambo muhali, wengine kunifukuza
Natafuta mwanamwali, nani tanielekeza?
Nimezunguka Mombasa, mji wote nimepita
Pale pa kutoa posa, hakika sijapapata
Kivipi nimemkosa? yule wa kuniambata
Nambieni langu kosa, ni wapi nitampata?
Nilipeleka salamu, watu hawakuiitika
Nimeenda pia Lamu, visiwani nimefika
Ila sasa sifahamu, kwa nini sijaridhika?
Na pia kule Watamu, mambo yamevurugika
Safari yangu ya Vanga, dafu kweli sikufua
Mchumba kwenda kuzinga , sikueza mfichua
Yamekuwa ni majanga, sasa ndio natambua
Ndoa bila kuipanga, ni dhoruba ya kifua
Menichosha ukapera, kitu gani cha kufanya?
Natafuta mke bora, wapi nitamkusanya?
Mzuri hulka na sura, wastani na mwenye mwanya🤗
Munipe na hio dira, nende wapi hii Kenya?
Alhamdani Mohamed
Kalamu Dumu Daima
