Ajabu yenye ajabu, kwetu sisi waislamu
Aibu tena aibu, vipi tutajifahamu
Ni zipi hasa sababu? kila leo kulaumu
Dada muvae hijabu, kwenu ni pambo muhimu

Ewe binti taratibu, punguza wako wazimu
Kisome chote kitabu, liwe ni lako jukumu
Uwe mwingi wa adabu, mpole na mkarimu
Dada muvae hijabu, kwenu ni pambo muhimu

Vazi ukilighilibu, huko ni kujidhulumu
Wangojewa na adhabu, kwa Mola wetu Hakimu
Ukiwa mstaarabu, watu watakuheshimu
Dada muvae hijabu, kwenu ni pambo muhimu

Isiwe kwako sababu, ya kungia jahanamu
Pigana na masaibu, yatokayo kwa ghulamu
Watenge kando shababu, vazi lako waheshimu
Dada muvae hijabu, kwenu ni pambo muhimu

Alhamdan Mohamed
Kalamu Dumu Daima

Categorized in: