Katika ya makutano, kuna matuko na njeo
Na mwia wa mapambano, vipambane hivi leo
Iwe kazi kwa mkono, kupepeta na uteo
Ai,ndewe na sikio, na njeo za makutano.

Ai,sikio na ndewe, msikizi aambwapo
Yasingekuwa ni wewe, mla yamini kiapo
Pambana nayo mwenyewe, ngama tezi omo upo
Ai,yowe na kilio, na njeo za makutano.

Ai!kilio na yowe, na mfumi afumapo
Nyama humla nyama we, akanyea mbingu popo
Simwambie hata nawe, akifuma uli upo
Ai,msasi na windo, na njeo za makutano.

Ai,Windo na msasi, alokubuhu kusaka
Siku anasapo gwasi, mtegoni kumshika
Kama mwasi aloasi, hata utu humtoka
Ai,ndaa na kiliwa, na njeo za makutano.

Ai,kiliwa na ndaa, na mwida wa kufuturu
Tende moja bila taa, na kizani hushukuru
Hadi tumbo likijaa, ndipo mwanga kuuduru
Ai,moyo na mahaba, na njeo za makutano.

Ai,mahaba na moyo, na mpendi akipenda
Huwa ni wivu na choyo, kwa mtendi na kutenda
Mahaba unipendayo, kiniacha tawa ng’onda
Ai,mawazo na bongo, na njeo za makutano.

Ai,bongo na mawazo, na shinikizo yajapo
Yajapo na shinikizo, pipa huliona kopo
Kigongo huita nguzo, na ingawa nguzo ipo
Ai,pipi na mtoto, na njeo za makutano.

Ai,mtoto na pipi, mdomonimwe na mate
Mwambie kwamba humpi, aanze vita mtete
Hwamba alizwa n’kipi, hata kulia kwa kite
Ai,kilio na chozi, na njeo za makutano.

Ai,chozi na kilio, kwa mwenye nalo kushusha
Kikawa kisingizio, ngawa mambo yamekwisha
Huwika ungamba kwio, mawio kutuamsha
Ai,kiguu na ndia, na njeo za makutano.

Ai,Ndia na kiguu, msafiri na safari
Kiguru ana nafuu, hata gari huabiri
Kifika juu ya nguu, kafurahi mandhari
Ai,mwisho na kikomo, na njeo za makutano.

Rashid Mwaguni.
8/Ramadhan/1441
1/5/2020

WRITER – RASHID

Categorized in: