Mwanangu
Taali keti kitako, maneno kukuambiza
Yakae kichwani mwako, vizuri nisikiliza
Ingawa mwa mboni zako, bado kuna kingi kiza
Taali ewe mwanangu

Mwanangu
Nafanya uradi huu, kipenzi kukuusiya
Kwa kuwa sina ujuu, simi wa kuijuliya
Siku ya kwenenda juu, roho hii nilopewa
Ninakhofiya mwanangu

Mwanangu
Ni kweli u kinda sana, nasadiki, ninajuwa
Huu wako uvulana, sio ule wa kuowa
Ila ni bora kunena, ningali ninapumuwa
Unielewe mwanangu

Mwanangu
Ungali kwenye makuzi, mwana zingatiya hili
Udume si uchafuzi, tafadhali tafadhali
Siyafanye ya ajizi, tambuwa Mola halali
Angusha macho mwanangu

Mwanangu
Anza sasa kuzishika, za nawafili swaumu
Vigengeshari epuka, haina jema kaumu
Pindipo ikikucheka, usiingiye wazimu
Sifisidike mwanangu

Mwanangu
Tena kwenye funga zako, dumu kuleta duaa
Tawasuli peke yako, faraghani ukikaa
Ufike wakati wako, mudao wa kuliwaa
Kiwa msafi mwanangu

Mwanangu
Na yashike ya Rasuli, kwenye vigezo vinne
Mwenye dini na jamali, akija usimkane
Hata nasabu na mali, navyo hivyo uvione
Sikengeuke mwanangu

Mwanangu
Ila tambuwa kwa dhati, ni vigumu tena sana
Mmoja kumthibiti, vigezo vikakutana
Uwe wa kati kati, penye dini shikamana
Pa dini ndipo mwanangu

Mwanangu
Lakini hata uzuri, nao una umuhimu
Huo hupoza ghururi, zao hao wanadamu
Hakikisha wamjiri, kupoza zako fahamu
Uzuri dawa mwanangu

Mwanangu
Na usifanye ubishi, kwa huo kujingojeza
Uzuri ni kama moshi, huwezi kuubakiza
Tena wazuri haweshi, na wema wanamaliza
Nizingatiya mwanangu

Mwanangu
Keti kando na papara, ili usijepoteya
Ziswali istikhara, Mola kumuuliziya
Pia na istishara, ni amali ya sawiya
Ona wavyele mwanangu

Mwanangu
Na Mola akikujibu, kwa kukupa alo mwema
Shukurani kwa jawabu, ni duaa za daima
Za kumuomba Mujibu, awadumishe salama
Kudumu kazi mwanangu

Mwanangu
Tamati usijewata, kumuomba auladi
Wale wasio matata, usikauke fuadi
Akupe wenye kukita, kwenye diniye Wadudi
Wakuliwaze mwanangu


Abuw Haytham, Bashiru Abdallah
Magole, Dar es salaam – Tanganyika
Alhamisi, 17/06/1443, 20/01/2021

Categorized in: