Penzi ni dawa jamani, hutibu shida na dhiki
Penzi ni lulu moyoni , tambua hili rafiki
Penzi lako la thamani, kwengine halishikiki
Penzi ni tiba mwilini, hutibu kila hisia

Penzi hutibu mtima ,’kipata mwema tabibu
Hutibu mwili mzima, ushikwapo masaibu
Penzi lako la heshima, hutibu kwa taratibu
Penzi ni tiba mwilini, hutibu kila hisia

Penzi ni kama zawadi, hili kwako nalisema
Penzi ua la waridi, natamani kulichuma
Penzi kwako likizidi, hupoa gonjwa la homa
Penzi ni tiba mwilini, hutibu kila hisia

Penzi lilo la asali, milele kwangu hudumu
Penzi ni jambo aali, kulilinda ni muhimu
Penzi kwako ni sahali, hili jambo lifahamu
Penzi ni tiba mwilini, hutibu kila hisia

Penzi ni la wale watu, wapendanao kikweli
Penzi si kitu ni utu, wa kila hali na mali
Penzi lako si kiatu, cha kwenda kila mahali
Penzi ni tiba mwilini, hutibu kila hisia

Alhamdan Mohamed
Kalamu Dumu Daima

WRITER – HAMDHAN ABDALLAH

Categorized in: