Japo kutunga kugumu,na si rahisi wajua
Thamani yako muhimu,almasi dhahabia
Imenipa ilhamu,Radhia kukutungia
Ozi la mwezi Radhia.

Kama mbingu ya nujumu,imetavyo kilimia
Na tabasamu adhimu,wajihi likipasua
Ndo ulivyo mhashamu,hunikosha maridhia
Ozi la mwezi Radhia.

Mbora intidhamu,rihi waridi kilua
Radhia wangu fahamu,moyoni umeningia
Naomba nipe hatamu,ubebe zangu hisia
Ozi la mwezi Radhia.

Rutuba dongo kinamu,unawirivyo mmea
Huba lako muadhamu,ndivyo nilivyolilea
Tunda ule tunda tamu,tufaha tunda murua
Ozi la mwezi Radhia.

Kila cha kwako kitamu,ni nini tende halua?
Kwa urembo na nidhamu,maadili na tabia
U mwema u mkarimu,sioni wa kufikia
Laiki yako Radhia.

Songa basi nkushumu,kama umeniridhia
Nyoyo zipane salamu,zipate kufurahia
Nikumbate kiwazimu,ka pua na kupumua
Ozi la mwezi Radhia.

Sinitoe milizamu,huzuni chozi kulia
Kuwa moyo niwe damu,mwili uwe na afia
Au jua la Rahimu,wangaze yetu dunia
Ozi la mwezi Radhia.

Laazizi nna hamu,na ghamu kuendelea
Ila ya kwangu kalamu,wino imejiishia
Mahabuba wasalamu,salamu zangu pokea
Ozi la mwezi Radhia.

© Rashid Mwaguni

WRITER – RASHID

Categorized in: