Hatwawi korokoroni,mwinyi maguvu mkwasi
Kuziwiwa kifungoni,kwake yeye haipasi
Ilitengezwa kiini,iwe ni ya kwetu sisi
Jela ni ya masikini,tajiri hana nafasi.

Waibe mabilioni,viwango viso kiasi
Nchi kuitia deni,na uchumi wa nakisi
Wala hawawekwi ndani,na kufunguliwa kesi
Jela ni ya masikini,tajiri hana nafasi.

Mwizi wa kuku harani,hwandikiwa wadadisi
Mnyonge hana hanani,kisha wakamfilisi
Na kukicha hali duni,maisha ni mwendo kasi
Jela ni ya masikini,tajiri hana nafasi.

Umero serikalini,waja wamekuwa fisi
Mali ghushi tani tani,kufanyia umilisi
Hawinde yu taabani,kisa kaiba adesi
Jela ni ya masikini,tajiri hana nafasi.

Wavamizi mashambani,na kuzifisha nafusi
Kisa wapate madini,dhahabu na almasi
Kuwafidi hawaoni,masikini kisa gesi
Jela ni ya masikini,tajiri hana nafasi.

Ni majanga aushini,kushindia mafenesi
Kule wala biriani,makuku na katlesi
Ni mnyonge mnyongeni,rafiki yake risasi
Jela ni ya masikini,tajiri hana nafasi.

Pengo hili siku gani,litapunguka kiasi
Sheria zetu kortini,ziwe haki taasisi
Uhuru uraiani,ufike kwetu rahisi
Jela ni ya masikini,tajiri hana nafasi

Natia nanga mwishoni,sendelei hapa basi
Si kutunga tungo hini,ni kuwa yamenighasi
Masikini hadi lini,tafanywa kikaragosi
Jela ni ya masikini,tajiri hana nafasi.

Rashid Mwaguni.

WRITER – RASHID

Categorized in: