Moyo nyamaza kulia,umshukuru Rabuka
Ingawa mekulemea,mazito ya kila rika
Shukuru ndiyo dunia,huwa kupanda kushuka
Kwinamako huinuka.
Moyo kaza vumilia,nusurayo itafika
Najua yana udhia,na hakika umechoka
Mwangaza utatujia,pa giza patakunduka
Kwinamako huinuka.
Moyo usende chukia,ya mapyoro ukafoka
Haitakusaidia,dhiki haitaondoka
Ila njema nia tia,uuondoshe wahaka
Kwinamako huinuka.
Ni mipango ya Jalia,kila jambo kutendeka
Kila linapotukia,huwa yeye ametaka
Sasa mtima tulia,nawe utafurahika
Kwinamako huinuka.
Najua unaumia,kwa dhiki ya kudhikika
Zito lilokufikia,gumu sana kubebeka
Dawa ya tamaa tia,jaraha litaponyeka
Kwinamako huinuka.
La simanzi kujitia,hadi chozi likashuka
Si suluhu nakwambia,mtima wangu zinduka
Heri ukasubiria,Muumba mbingu tabaka
Kwinamako huinuka.
Futa chozi kalbia,utoe na zako shaka
Mola tatusahilia,palofungwa hufunguka
Kila hatua ni dua,tuombe tutasikika
Kwinamako huinuka.
Ni heri hapa kutua,na nukta kuiandika
Yangu niliyotongoa,moyo wangu basi shika
Utaiona afua,na hali kuimarika
Kwinamako huinuka.
Rashid Mwaguni
RMM
WRITER – RASHID
