Wakenya ninalo swali, nijibuni kwa makini,
Lanisumbua akili, mwenzenu sina amani,
Hivi muonavyo hali, huwa mnawaza nini?
Maovu kupendelea, tunajenga nchi gani?

Ufisadi kawaida, umetwingia damuni,
Tutaki kulipa ada, tunapenda chinichini,
Unavyosongea muda, wana watarithi nini?
Maovu kupendelea, tunajenga nchi gani?

Wizi nao unyang’anyi, hatutaki kukemea,
Tunajitia umanyi, twaita kuangukia,
Kama tutoi mikanyi, itawaje kwendelea?
Maovu kupendelea, tunajenga nchi gani?

Siasa ni za matusi, hadi yale ya nguoni,
Tunatumia kamasi, sio akili vichwani,
Takapozuka uasi, tutaendapi jamani?
Maovu kupendelea, tunajenga nchi gani?

Twanyonya rasilimali, ni kama kesho haipo,
Mazingira hatujali, tunaishi kama popo,
Mbona tusiwaze mbali, kwavyo vizazi vichapo?
Maovu kupendelea, tunajenga nchi gani?

Mashoga na wasagaji, hadharani twatangaza,
Ma’dili ukiukaji, eti kujiendeleza,
Ndugu zangu wasomaji, huko siko kuteleza?
Maovu kupendelea, tunajenga nchi gani?

Twasifia ukabila, badala ya uzalendo,
Mpaka vyombo vya dola, huo huo nd’o mwenendo,
Huo ukitutawala, tapata wapi upendo?
Maovu kupendelea, tunajenga nchi gani?

Nimeyataja machache, ila mengi mwayajua,
Tusiyangoje yachache, nchi kituvunjikia,
Ni heri tuzime cheche, moto sijetuwakia,
Maovu kupendelea, tunajenga nchi gani?

Allan Lumunyasi Chevukwavi.
Mwoshashombo.
Nairobi.
WRITER ALLAN CHEVUKWAVI

Categorized in: