Wenye vyeo tazameni, mambo yamebadilika
Maisha ni hali duni, na uchumi unashuka
Ni nakisi kwa madeni, na bei zimefumka
Huyu punda amechoka, tazameni masikini.

Halionekani peni, ingawa tunalisaka
Halikai mifuko ni, hupotea kwa dakika
Nazo bidhaa sokoni, uchao zinaghalika
Huyu punda amechoka, tazameni masikini.

Mapesa mabilioni, yaibwa yaangamika
Maendeleo nchini, ni ndoto isotimika
Miradi hatuioni, haiwi kumalizika
Huyu punda amechoka, tazameni masikini.

Tutalia hadi lini, huyu punda amechoka
Mzigo unamhini, maishani adhikika
Apatepi ahueni, na kwake ni kumenyeka
Huyu punda amechoka ,tazameni masikini.

Mafuta yako paani, bei yake imefika
Mnyonge hana hanani, kwake ni kudhulumika
Mikakati ifanyeni, wanyonge tunateseka
Huyu punda amechoka, tazameni masikini.

Mapato yenda kizani, ushuru waongezeka
Mimali ya umma Tani, mwaiba mnalundika
Dhuluma ni haki gani, mnyonge ananyongeka
Huyu punda amechoka, tazameni masikini.

Wakubwa wangalieni, uchumi huu wa shoka
Watuchanja kama kuni, vipande tumepasuka
Huruma tuoneeni, mayahe twadhalilika
Huyu punda amechoka, tazameni masikini

Sikuupaza uneni, ila ni kusikilika
Sie huku mashinani, twaumia tumechoka
Nyendo zibadilisheni, nchi itaporomoka
Huyu punda amechoka,tazameni masikini.

© Rashid Mwaguni

Categorized in: