Zilipomoka zidaka, zikaacha nazi pevu
Mbumbumbu akaongoka, akapotoka mwelevu
Haikunya ya masika, hari ikanya kwa nguvu
Mtoto kamea ndevu, kipya kikamea kuvu.
Sufi zilivunja shoka, na jiwe likawa jivu
Misitu ikakauka ,ikamea jangwa kavu
Mnyonge alodunika, leo ni mwinyi maguvu.
Mtoto kamea ndevu, kipya kikamea kuvu.
Yule alovuvumka, amepatwa na kivumvu
Mzima tukamzika, mgonjwa ashuka shavu
Pametakata pa taka, pasafi paona wivu
Mtoto kamea ndevu, kipya kikamea kuvu.
Kipusi chaua paka, kimemkata ubavu
Zohali kazi ataka, amekimbia uzivu
Mabichi yameanguka, yamebakia mabivu
Mtoto kamea ndevu, kipya kikamea kuvu.
Chang’aa chamemetuka, chang’aa chuma chakavu
Kilo’wa kimetupika, kinameta niking’avu
Lisiloyumkinika, leo lawa elekevu
Mtoto kamea ndevu, kipya kikamea kuvu.
Alozikwa amezuka, laongea lake fuvu
Nyaka haina baraka, watoka mbio utomvu
Jagina ana wahaka, si tena mkakamavu
Mtoto kamea ndevu, kipya kikamea kuvu.
Yule aliyesifika, leo amebwagwa chavu
Chini anaweweseka, kama kaumwa na mavu
Amenaswa kanasika, haopoki huu wavu
Mtoto kamea ndevu, kipya kikamea kuvu.
Pa hatima nimefika, sasa navua glavu
Sendelei nimechoka, nimekuwa mziavu
Mkono unakunjika, kama kwamba mlemavu
Mtoto kamea ndevu, kipya kikamea kuvu.
Malenga ”Mte Tipuzi”
Rashid Bin Mwaguni.
