Siku ya tua na twika, msi ozi akiona,
Pachimbwa patachimbika, utafukuka na mwina
Siri itabainika, bayana kama mchana
Msi ozi akiona, siku ya tua na twika.
Siku ya tua na twika, akikua nyuki jana
Mrina utaumbuka, mrina uki mrina
Taumwa atafutuka, na sega hataliona
Akikua nyuki jana, siku ya tua na twika.
Siku ya tua na twika, siafu wakiungana
Tawa taabani nyoka, atataataa sana
Shimoni asipotoka, atafa humo naona
Siafu wakiungana, siku ya tua na twika.
Siku ya tua na twika, msi jino kitafuna
Minyama ikichanika, fupa akiliguguna
Genderi talainika, na itatafunwa sana
Siku ya tua na twika, msi jino kitafuna.
Siku ya tua na twika, mtu bubwi akinena
Kihutubu na kufoka, yote yalorundikana
Palokombo patanyoka, palopinda kupindana
Mtu bubwi akinena, siku ya tua na twika.
Siku ya tua na twika, mwana akizaa mwana
Jira hizo zitafika, kuwe mkembe hakuna
Ndipo utajua fika, dunia si yako tena
Mwana akizaa mwana, siku ya tua na twika
Siku ya tua na twika, kila mtu mbona!? mbona!?
Ndipo watakukumbuka, mambo yatakapobana
Sura zitatebwereka, kwa soni wakisonona
Kila mtu mbona? Mbona? siku ya tua na twika.
Siku ya tua na twika, na wino usipotona
Sipotona kuandika, nikupangie na vina
Utatamani kutaka, nitunge japo sivina
Na wino usipotona, siku ya tua na twika.
Siku ya tua ya twika, buriani muungwana
Mwisho wangu ukifika, niwe cha kusema sina
Mdhukuri akiweka, yatamwauni awana
Buriani muungwana, siku ya tua na twika.
© Rashid Mwaguni
WRITER – RASHID