Wake wengine ni jaha, nuru shani ya Manani

Wamejaliwa staha, na utu uso kifani

Nyumba hutia furaha, furaha  na farahani

Nuru shani ya Manani, wake wengine ni jaha 

 

Wake wengine mizaha, kwa kujawa na utani

Kwamba kucheka ndo siha, mazidadi si maani

Hata kwa mtu maliha, hugeuka mtu duni

Kwa kujawa na utani, wake wengine mizaha. 

 

Wake wengine ni siha, mume kuwa afueni

Ukipata majeraha, moyo kuwa vidondani

Huukamua usaha, ukapoa mwafulani

Mume kuwa afueni, wake wengine ni siha 

 

Wake wengine silaha, hupambania vitani

Kwa ghadhabu na kariha, na utesi wenye kani

Hulipuka kama zaha, wakati wa Volkani

Hupambania vitani, wake wengine silaha

 

Wake wengine majuha, wapuuzi nje ndani

Hawakomeki kuhaha, si sekunde si kuruni.

Wape kizuri tufaha, watakitupa chooni

Wapuuzi nje ndani, wake wengine majuha 

 

Wake wengine mashaha, wamebobea fanini

Watungao ufasaha, tungo ziso nuksani

Wamejaliwa nasaha, na busara za waneni

Wamebobea fanini, wake wengine mashaha. 

 

Wake wengine karaha, nuhusi na visirani

Hawadumiki nikaha,hata vyuo ishirini

Kwa nyota yao ya mbweha, kuzururia mwituni

Nuhusi na visiwani, wake wengine karaha. 

 

Awaongoe illaha, walopotoka njiani

Nawaomba msamaha, nilowakwaza moyoni

Imenikoma kariha, nakomeka kikomoni

Wake wengine ni jaha, wake wengine karaha. 

 

Rashid Mwaguni

WRITER – RASHID

Categorized in: