Kati ya malengo ya SHIWAKI, moja ni kuwajengea uwezo waandishi wa lugha ya Kiswahili katika uandishi wa tanzu mbalimbali za fasihi ya Kiswahili hasa kupitia njia rahisi ya teknolojia ya mikutano ya mtandaoni.
Tunakumbuka jumamosi ya tarehe 11 Juni 2022, chini ya SHIWAKI kulifanyika warsha ya kwanza ya mtandaoni. Warsha hii ilijikita katika kujifunza namna bora ya kuandika mashairi ya Kiswahili ambayo iliendeshwa na Bashiru Abdallah akiwa kama muongozaji sambamba na Mohammed Ghassan akiwa kama mgeni na msemaji mkuu.
Kwa mfululizo huu wa matukio haya, mnamo tarehe 04 Septemba 2022 sawa na siku ya Jumapili, kutakuwa na warsha nyingine ambayo itajikita zaidi katika kuelezea namna bora ya uandishi wa riwaya kwa lugha ya Kiswahili.
Tunatarajia kuwa na Bi. Anna Samwel kama mgeni. Anna Samwel Manyanza ni mwandishi wa riwaya na hekaya za watoto. Amezaliwa na kukulia mkoani Tanga lakini kwa sasa anaishi nchini Uswisi na familia yake. Anna ana shahada ya Uzamili ya Siasa, Lugha na Uandishi wa Habari kutoka Chuo Kikuu cha Leibniz Universität Hannover, Ujerumani. Riwaya yake ya Penzi la Damu imechukua ushindi wa kwanza kabisa wa Tuzo ya Mabati Cornell ya Fasihi ya Afrika, 2015. Kakofia Keusi ni hekaya yake ya kwanza ya watoto ambayo imebahatika kufasiriwa katika lugha ya Kingereza, Kijerumani na Kifaransa. Agosti 2022 amewasilisha kazi zake katika warsha ya kimataifa ya Waandishi wa Afrika iliyofanyika jijini Berlin, Ujerumani.
Muongozaji wa warsha hii atakuwa ni Bw. Shisia Wasilwa. Shisia Wasilwa ni mwanahabari na mwandishi wa kazi za fasihi. Shisia ni mhariri katika kituo cha KTN nchini kenya. Amehudumu na mashirika ya habari ya KBC, Citizen Tv, China Radio Kimataifa, BBC na Deutsche Welle. Ndiye mwandishi wa riwaya za Dunia Tambara Bovu, Makovu ya Uhai na Kengeza la Jasiri mbali na kuhariri kazi nyingi za fasihi ikiwemo kazi ya marehemu Ken Walibora ya Ndoto ya Almasi. Kwa sasa anazamia shahada ya Uzamili katika masuala ya habari na teknolojia katika Chuo Kikuu cha Aga Khan nchini Kenya.
Warsha hii itafanyika kupitia mtandao wa “Google Meet” kuanzia saa kumi na dakika thalathini jioni na kumalizika saa kumi na mbili jioni.
Uzi wa mkutano huu utapatikana kwenye tovuti yetu sambamba na majukwaa yetu ya mitandao ya kijamii.
Usikose!!
