Kila lilokuwa zuri, kulipata ni muhali, mie nimeshadadisi
Mwanzo huwa ni shubiri, ya uchungu mara mbili, pamwe nao ukakasi
Aliye nazo kathiri, hazina za amuwali, hazikuja kirahisi

Huyo alitabahari, kwazo juhudi za kweli, pasi kusema khalasi
Hadi tamu kudhihiri, kwa kuirina asali, katu hakunena basi
Ukiyataka mazuri, juwa hakuna sahali, zitakutoka kamasi

Ili nyota kudhihiri, mara nyingi utafeli, ujione na nuhusi
Kizuri hakina siri, vikwazo sipokabili, matokeo huwa hasi
Mabaya usitabiri, utaichosha akili, na kuharibu nafasi

Simama uwe ngangari, tazama jicho la mbali, tenda kwa mwendo wa kasi
Muweke mbele Qahari, vazi lako tawakuli, uturio ikhilasi
Hapo licha ya kikiri, na mambo yenye muhali, ni hakika utapasi

Ijumaa, 07/11/1439, 20/07/2018


Diwani: Wino wa Dhahabu (uk. 140 – 141)
Mtunzi: Bashiru Abdallah (Abuw Haytham)
Mchapishaji: Fanani Mpole Printers, Dar es salaam

WRITER – Bashiru Abdallah

Categorized in: