Kwenye magwa yagwishayo, mbwagwa akaanguka,
Mgwa magwa abwagwayo, akagwa kutoinuka,
Gwisho la yake magwiyo, mgwa anapopomoka,
Ukigwa mgwa nyanyuka, kugwa kuwi kutokwima
Kugwa ukibwagwa mbiyo, sijikawize zinduka,
Usibwagike magwayo, kama ugwe ama nyoka,
Kigwa maguu unayo, ugwapo mgwa inuka,
Ukigwa mgwa nyanyuka, kugwa kuwi kutokwima.
Ungabwagika pekeyo, nishati mekutindika,
Yatazame magwa yayo, magwayo ukidondoka,
Winue na maganjayo, umhimidi Rabuka,
Ukigwa mgwa nyanyuka, kugwa kuwi kutokwima
Umegwa una kilio, eti chozi lakushuka!
Kilia machozi yayo, maozi yamezibika,
Utayonaje wendayo, ndiayo uliyoshika,
Ukigwa mgwa nyanyuka, kugwa kuwi kutokwima
Kiduchu changu n ambayo, inuka ukibwagika,
Kigwa sipige miayo, jidomo limepanuka,
Hayo ya kukaa siyo, ukichoka shajiika,
Ukigwa mgwa nyanyuka, kugwa kuwi kutokwima
Nilokugea mageyo, yagwiyeto ukigwika
Usijegwaya keshoyo, magwani ukipweteka
Ni hayo sina zidiyo, utapogwa haya shika
Ukigwa mgwa nyanyuka,kugwa kuwi kutokwima.
© Rashid Mwaguni
WRITER – RASHID
