Niliibofya honi ya gari langu, baada ya dakika mbili hivi. Nikafunguliwa lango na bawabu wetu Bwana Maasai Mrefu. Maasai alikuwa amejifunga lubega, kisu kiunoni na kimangare mkononi. Ama kweli, alikuwa amejihami kutulinda. Tulimwamini mno kutoka na ujasiri wa kupambana na wezi. Baada ya salamu. Nilimuaga. Nilipanda vidato polepole kama ilivyokuwa desturi na kawaida yangu. Sikupenda kupanda kwa haraka. Nilizingatia mno haraka haraka haina baraka. Tangu nilazwe hospitali kwa ugonjwa wa kifua kikiuu, mapafu yangu huwa hayastahimili kasi. Taratibu hadi gorofa ya nne, nilipoishi – mtaa wa Kakakuona – gatuzi la Kileoleo. Nilipofika orofani, nilishika ushoroba hadi mlangoni pangu nambari nne A (4A). Kupitia dirishani kama nilivyozoea sikuona mwangaza chumbani humo. Nikaitazama kopo langu la saa mkononi. “saa tano kasoro dakika kumi” kwani leo Aziza Karembo alilala mapema? Watoto wangu je? Wavulana wangu wawili: Juma na Jomo huwa ni nadra walale kabla sijafika, walikuwa na mazoea kutazama vipi vyao katika runinga ya AKILI KIDS baada ya habari za saa tatu, huku wakiningoja” nikajisaili kimoyomoyo.
Nilikitoa kicha cha ufunguo, nikachagua ufunguo rasmi. Nikautia tunduni. Nikaugeuzageuza ila ile sauti ya kufunguka kwa kitasa haikuwa. Nikautoa. Nikauangalia. Nikauchomeka tena tunduni. Wakati huu nikajaribu kuusukuma mlango. Mara ghafla, nikaanguka ndani. Kumbe mlango haukuwa umefungwa. kilichoushikila ni kijikaratasi kilichotiwa kwenye kizingiti na mlango ukafungwa kwa nguvu.
Sikuamini, nilitusatusa gizani. Nilipoipata swichi ya umeme. Nikaibofya. Mama yangu! Chumba kilikuwa kitupu. Chumba kilikuwa jangwa, chumba au niseme nyumba haikuwa na chochote wala lolote. Nilishangaa. Nilishtuka. Niliyakodoa macho. Vyumba vyote: Bafuni, jikoni, malazini. Ulikuwa uwanja, uwanja bila wachezaji. Haja ndogo ikanijia ghafla, nusra nijitabawalie. Nikaelekea msalani. Nilipomaliza kujisaidia. Karibu na mlango, nikakiona kijikaratasi. Kijikaratasi kilikuwa kimekunjwa ovoovyo. Nilikikunjua huku nikitetemeka. Vilikuwa viwili: Kimoja kilikuwa Ankara ya baani, maandishi ovoovyo: Pilsina -200/-, Taska….180/-, Kingfisha – 200/—- mhudumu alikuwa Caro. Ya pili ilikuwa risiti ya vyumba vya malazi nilipopopewa baada ya kulipia huduma siku tatu zilizopita. “Risiti hizi mbona niliacha nimeziteketeza. Imekuaje ipo hapa. Ama ilisahaulika kwenye suruali yangu ya dengirizi. Kumbe! Nilichoteketeza ni risiti ya benki pekee? Nijibiwe na nani? Ilhali nipo peke yangu?” Maswali mzomzo yalinijaa akilini. Kama wasemavyo nilijua nimepatikana. Janja kapata janjaure. Siku za mwizi zilikuwa zimetimia arubaini.
Nilileuka, pombe iliniisha kichwani. Maswali anuwai ubongoni. Binti wa watu nimemkosea nini? Tumeoana kwa miaka nane sasa. Tulikuwa tukikosana hapa na pale ila tulikuwa tunasameheana. Wapo wapi? Wametekwa nyara? Maswali ya nini na kwa nini? Yalinisumbua mno akilini. Nilijiiegemeza ukutani. Kisa na maana hapakuwa na mahali pa kukalia. Nikaichomoa simumaizi yangu. Nikaichakurachakura huku nikiitafuta nambari ya mpenzi wangu. laini zote hazikuwa na mjazo: Safaricom na Airtel. Ikabidi ninue mjazo kwa njia ya M-pesa. Mjazo ulipothibitishwa, ulimezwa. Kumbe nilikuwa nimekopa mjazo. Majanga juu ya majanga. Nikakopa tena shilingi mia moja. Nikaipiga tena nambari ya ahali wangu. Simu ilikiriza. Mkirizo uliandamana na wimbo wa Taarab wa Khadija Kopa.. Utalijua jiji.. mahadhi na mistari wimboni yalinigonga kama nyundo kichwani. “Mama mwimbaji huyu kaniimba kweli, leo ni leo, maudhui ya wimbo leo ni yangu” nikajisemea kimoyomoyo.” Sema mke wangu akaitika” Aziza (kwa kinyonge) mlienda wapi? mlihama bila kuniambia? Mpo wapi? Nikauliza.” “Sitaki maswali , wiki nzima ulinidanganya ulikuwa kazi eneo la pwani. Leo hii ukweli umethibitika. Nikifua nguo zako ulizokuwa nazo safarini. Niliziona risiti nyingi tuulizozitumia ukiwa kwenye hoteli ya kifahari ya Rahaleo. Niliichukua simu risitini nikawapigia. Yote wamenielezea. Wewe ulikuwa na kidosho Amina. Niliambiwa si mara ya kwanza kuenda pale. Wewe ni mteja wao. Mwanaume tafadhali mimi naogopa magonjwa. Mimi nayapenda maisha yangu. Isitoshe, nimewapigia tena nikajifanya mimi ni Amina, nikadai nilisahau kitu pale hotelini. Mwamume wewe ni gumegume . Wewe ni jogoo tuachane kwa amani. Nenda kwa Amina wako. Tulioana ukiwa huna hata kitu. Baada ya kuwa mtu sasa waniona kutu. Nimevumilia sana. Kulia usiku kucha. Tafadhali usinipigie simu tena. Ukiwataka watoto nitakuletea” Simu ikafyuka.
“Mama yangu! Moyo ulihama kifuani. Maneno yakaniuka kinywani. Siku za mwizi ni arubaini. Leo nimepatikana. Leo mambo ni wazi kama kizima. Nitajinasua vipi?” nikawaza mawazo moto kichwani.
Sakafuni. Nguo zangu zilikuwa zimetupwa ovyoovyo. Si shati si chupi si….kila aina ya nguo yangu ilikuwa pale. Zilizokuwa chafu, zilizolowa maji na safi. Nilijizatiti kiume nakuzizoazoa kila moja nikaiweka mahali pake. Safi nikarudisha shubakani. Chafu na zilizotota maji nikazirusha bafuni angalau kuzifua baadaye ama kuzipeleka dobi.
Nikarudi tena sebuleni. Nikaketi chini. Nilikuwa na wakati mzuri sana na Amina.Dada huyu nampenda sana. Kimwana huyu hunituliza mno. Amina anafanya kazi kama mhazili katika kampuni yetu. Mimi binafsi nilichangia mno kuajiriwa kwake. Ni kodosho wa sura. Sura baidhati. Macho malegevu urembo binti huyu amepewa. Nikaifungua simu yangu. Niliitafutafuta picha yake. Binti huyu ataniua kweli. Ila sasa naona ni kama nyani hapa ametembea sokoni mchana.
Mawazo yangu yafutika ghafla nilipouona utupu wa chumba changu. Niliwaza watoto wangu. Juma yupo gredi ya sita. Jomo yupo gredi ya tatu. Nilikuwa na mipango mizuri kuhusu wana wangu. Juma alionesha kipawa cha kuwa mhandisi. Jomo alionesha kipaji cha uimbaji. Ni shabiki sugu wa nyimbo za Bongo hasa kundi la WASAFI-anampenda sana mwanamziki Rayvanny. Wakati huo nilikuwa nariaria chumbani kama mwenye chungu mekoni. Wazo likanijia nimpigie binti Amina simu. Nilipojaribu kutafuta, simu ilikuwa imezimwa. Ama kweli, siku za nyani kufa miti yote huteleza. Nifanye nini tena? Njaa ilikuwa inaniuma sana.
Liwalo na liwe, nikaamua kutoka nje nitafute klabu chochote ninywe chupa pamoja na kizibo chake angalau nitulize kichwa changu. Nikakichukua kicha changu cha funguo. Nikaufunga mlango kwa komeo tu. Nikateremka vidato hadi maegeshoni. Gari langu nilikuwa nimeliegesha kando kabisa na magari mengine. Niliingia ndani .Niliutia ufunguo. Bawabu Masaai alijaribu kuongea nami lakini wapi? Akanifungulia lango na mimi huyoo nikielekea nisikokujua. Barabarani kulikuwa kweupe, nilipishana tu na mbwakoko na nunda pekee. Nililiendesha gari barabarani. Mziki garini ulitema cheche sawasawa. Nilikuwa naelekea upande palipokuwa na jiji kuu.
Kitalifa kidogo, nikapata kibao cha polisi. (POLICE CHECK) barabarani kilikuwa imekingamwa na vile vyuma vyao vyenye msumari. Nikasimamishwa. Polisi walikuwa wamejihami sawasawa. Watatu wakaja karibu na gari langu. Nikateremshwa kioo . “mzee wewe unaenda wapi? Wakati huu ni saa ngapi? Hujui ni wakati wa kafyu! Tena gari lako waliendesha vipi? Barakoa ipo wapi?” polisi wa kike akanifokea kwelikweli. Palepale akili ikarudi. Kweli serikali imetangaza kafyu kuanzia saa sita usiku hadi saa kumi asubuhi. Kafyu hii ni kwa sababu ya gonjwa la KORONA. Mara hiyohiyo. Nikaopolewa garini chapuchapu. “Kumbe wewe hata ni mlevi. Umekunywa wapi? Kazi yako ni kusambaza gonjwa hili.” Askari wa makamo wa kike akaniuliza. Jibu sikuwa nalo. Nilikuwa bubu. Nilibebwa hangahanga hadi kwenye karandinga liloegeshwa pembeni. Nilitupwa ndani kama gunia la makaa. Garini pia palikuwa na wateja wanne. Wanaume watatu na mwanamke mmoja. Wote walikuwa wamejikunja kama kabeji. Mimi pia nikatulia tuli kama maji mtungini.
Pale garini, nilikumbuka maisha ya furaha nilipokuwa nayo na mke wangu. Nilikumbuka tukiwa tunajivinjari ufukweni kule Pwani. Nilikumbuka jinsi mke alivyofurahia kuchezacheza na changarawe. Huku tukikimbizana na kuangushana kama vilebu. Upendo ulipokuwa moto. Wakati huo tulikuwa fungate.
Mawazo yangu yalikatishwa na mikikimikiki nje nilipochungulia askari walikuwa wanang’ang’a na mteja mwengine. Umoja ni nguvu alirushwa karadingani. Alikuwa mwanaume alikula akashiba. Aliingia kwa fujo nyingi. Alitusukuma na akaketi alipotaka. Kulingani na mwili wake. Sote tulinywea. Nani asiyejua angurumapo simba mcheza nani? Tena huyu asiogopa polisi? Mwanaume huyu. Alionekana amejaza hasira. Alifoka kwelikweli” wajinga hawa, wananishikia nini, mimi natoka kazini, nilikuwa nasaka riziki. Nisipoenda kazi watailisha familia yangu” sote tulimwangalia tu. Usemi wake ulikuwa na ukweli ila sheria ni msumeno ukata mbele na nyuma. Tujibu nini? Tena alivyoingia garini. Umjibu aruke nawe! Wacha tu.
Tulikaa pale karadingani kwa muda usiopungua saa tano. Baridi ilitukula kwelikweli. Anga ilimwaga mvua kwa hasira. Tulitetema kama jani la mgomba katika upepo wa kusi. Mimi binafsi nilikuwa nimevaa tu shati. Niliyaona ya kuona. Naam, ulimwengu hapa ulikuwa umenifunza bila huruma. Kimya chetu kilipasuliwa na sauti ya askari. Kila mmoja wenu anapelekwa karantini. Hii itakuwa funzo kwa wengine wanaokaidi amri za serikali na Wizara ya Afya. Pengine simu mlitewe nguo. Twawapeleka kituo cha karantini cha Neema Shule Ya Msingi. Hili la kupiga simu iliamshwa kovu moyoni. Nimpigie nani? Mke wangu ametoroka, ameenda kusikojulikana. Nitafanya nini ? Wakati huo jua lilikuwa limechomoza. Ilikuwa mwendo wa saa moja hivi. Wengi walikuwa wameletewa nguo. Mimi na yule mwanamke hatukuwa tumeletewa. Tulienda karantini na nguo zilizokuwa mwilini. Njaa niliokuwa nayo ilikuwa imetoweka.” Hawa polisi wataambiwa na nani? Malaika Jibrili si angalau awaeleze ninachopitia?” Nikajisemea kimoyomoyo. Nilizidi kutia dua.
Tulifika kituoni saa tatu asubuhi. Mapokezi hayakuwa yakupendeza. Kila mmoja alimwogopa mwengine. Tuliogopana. Kila mmoja anajitenga mbali na mwenziwe. Tuliambiwa tutakaa kituoni kwa siku kumi na nne. Tulichukuliwa vipimo vya kukagua kama tuna virusi vya KORONA. Mwili si wangu. Mawazo kichwani kama rangi ya lumbwi.” Familia yangu,gari langu, stakabadhi za kazi garini?” Si kuwa na la kufanya. Yote haya nitayafuatilia nikitoka karantini.
Mwandishi – Mwl. Eric Muteti
Maarufu kama Kaka Teitei
WRITER – Mwl Eric Muteti
