Ya hapa Kenya maisha, hayaishiki,
Chakula ukijilisha, hakilikiki,
Bei wameipandisha, haishukiki.

Dukani kukinunua, hakinunuki,
Gharama wameinua, haishukiki,
Kwa ushuru kwongezea, haupunguki.

Kijaribu kulalama, hausikiki,
Na huko kurudi nyuma, hakurudiki,
Maneno wanayosema, siyaridhiki.

Gesi pia imepanda, haijaziki,
Moshi wa kuni mkosi, huvumiliki,
Ni heri kuwa farasi, hausumbuki.

Serikali tunaomba, haiombeki,
Macho imeyafumba, hayafumbuki,
Tutegemee Muumba, atubariki.

Allan Lumunyasi Chevukwavi.
Mwoshashombo.

Categorized in: